logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Patanisho: Mwanadada alalamika kuibiwa mumewe na shemeji yake baada ya mume wake kufariki

Shantel alisema baba mkwe alimshauri mume wake achumbiane na mjane wa kaka yake alipofariki.

image
na Radio Jambo

Habari23 May 2023 - 05:37

Muhtasari


•Shantel alisema aligura ndoa yake ya miaka minne mwezi Machi mwaka huu baada ya kushuku mumewe anatoka kimapenzi na mkwe wake.

•Charles alipuuzilia mbali madai ya mkewe na kubainisha kuwa hana uhusiano wowote wa kimapenzi na mkwe wake.

GHOST NA GIDI STUDIONI

Bi Shantel Ndanu ,23, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Charles Mutinda ,30, ambaye alikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Shantel alisema aligura ndoa yake ya miaka minne mwezi Machi mwaka huu baada ya kushuku mumewe anatoka kimapenzi na mkwe wake.

Alidai mumewe alijenga ukaribu na mkwe wake baada ya kaka yake ambaye alikuwa amemuoa kuaga dunia.

"Mwezi Desemba mwaka jana mkubwa wake alikuja akafariki. Nilikuwa nyumbani pekee yangu. Wakati wa kupanga mazishi nilikuwa nyumbani pekee yangu. Mume wangu alikuja na bibi ya huyo kakake akarudi kisha Nairobi," alisema.

Alisema baada ya mkwe wake kuaga na kuzikwa, baba mkwe alimshauri aende Nairobi ili kukaa na mjane wake na kumsaidia kupamba na majonzi.

"Tuliongea na baba junior nikaenda. Nilienda Nairobi nikakaa mwezi moja kisha nikarudi nyumbani," alisimulia.

Alisema baadaye baba mkwe alianza kumshauri mume wake achumbiane na mjane wa kaka yake aliyefariki.

"Baba aliwaita (Charles na mjane) wakakaa chini na kuzungumza. Sikuhusishwa. Walikaa wakapanga waende kwa mganga kwa ajili ya maombi. Charles hakuniambia, aliniamsha asubuhi akaniambia wanaenda maombi," alisimulia.

Aliendelea, "Vile walitoka kwa maombi hatukuongeleshwa. Nikasema kama hawataki kuniongelesha ni sawa. Asubuhi iliyofuata waliamka wakarudi Nairobi."

Shantel alisema wakati akiwa kijijini, mume wake alikuwa anashiriki muda mwingi na mkwe wake na hata alilala kwa nyumba yao.

Alidai kwamba kuna wakati mumewe na mkwe wake walienda nyumbani pamoja, wakalima na kupanda chakula kisha wakaenda, jambo ambalo lilimkasirisha hadi akachukua hatua ya kuondoka na kurudi kwao.

Charles alipopigiwa simu aliahidi kwamba atamtafuta mkewe ili wapate kuongea na kusuluhisha mzozo wao.

Alipuuzilia mbali madai ya mkewe na kubainisha kuwa hana uhusiano wowote wa kimapenzi na mkwe wake.

"Hakuna uhusiano. Hakuna kitu inaendelea. Ni hasira nilikuwa nayo lakini nitamtafuta tuongee na yeye," alisema.

Alimhakikishia mkewe kuhusu upendo wake mkubwa kwake na akaahidi kumpigia simu  siku ya Jumatano.

"Bado wewe ndo bibi yangu, bado nakupenda," alisema.

Wawili hao walikubaliana kushiriki kikao na kusuluhisha mzozo wao.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved