Kusikizwa kwa kesi ambapo wachezaji wawili wa raga walishtakiwa kwa kosa la kubaka mwanamziki kumegonga mwamba miezi mitano baada ya washukiwa kula kiapo upya.
Hii ni baada ya Frank Wanyama mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo kuwasilisha ombi katika mahakama akitaka kesi hiyo kusimamishwa.
Wanyama ambaye ameshtakiwa pamoja na Alex Olaba alisema kwamba jaji Ngenye Macharia aliyeagiza kusikizwa upya kwa kesi hiyo alihujumu sheria katika uamuzi wake wa rufaa.
Kupitia kwa wakili Pravin Bowry, Wanyama alimwambia hakimu mkuu mkaazi Zainab Abdul kwamba anafaa kuacha kusikiza kesi hiyo na kuihamishia kwa mahakama kuu.
Wakili pia alisema kwamba tayari wamewasilisha kesi katika mahakama ya rufaa wakipinga uamuzi wa Jaji Ngenye na ombi la kusitisha kusikizwa kwa kesi hiyo bado lasubiri kuamuliwa mahakamani.
Wanyama anahofia kwamba kesi hii nyingine huenda ikaelekea katika hukumu nyingine kulingana na matokeo katika mahakama kuu iliyosema kwamba alifanya mapenzi bila makubaliano na mlalamishi hata ingawa ushahidi haukutolewa chini ya kiapo.
Pia anahoji kwamba kutokana na mifano ya awali kuwa maamuzi ya mahakama ya juu hayawezi kubadilishwa na mahakama ya chini, hakuna uwezekano kwamba hakimu wa mahakama ya chini atatoa uamuzi kinzani na ule wa mahakama kuu kuhusu hoja ya ushahidi.
Wakili wa Wanyama, Bowry anasema kwamba Jaji Ngenye bila kukusudia alimhukumu Wianyama kutokana na ushahidi ambao haukuapishwa kutoka kwa mlalamishi, ushahidi ambao jaji aliamua kwamba ulikuwa kuhujumu haki.
"Ngenye aliagiza kusikizwa upya kwa kesi hiyo kwa sababu kulingana na stakabadhi za kesi mlalamishi hakula kiapo kabla ya kutoa ushahidi wake," Bowry alisema.