HABARI NA GEORGE OWITI;
Watu watatu wamefariki huku wengine kadhaa wakipata majeraha katika ajali mbaya katika barabara ya Koma - Kenol kaunti ya Machakos.
Meneja wa Hospitali ya Kangundo Level 4, Evayo Loveto alisema miili tatu, miwili ya wanawake na mmoja wa mtoto imehifadihiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.
Walioshuhudia walisema watatu hao walikufa papo hapo baada ya gari lao aina ya probox kugongana ana kwa ana na prado kati ya Koma Hill na Kenol karibu na soko la Masokani katika Kaunti Ndogo ya Matungulu siku ya Jumanne.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Matungulu Monica Kimani alithibitisha kisa hicho.
Kimani, hata hivyo, alisema bado hajapata maelezo ya ajali hiyo kutoka kwa maafisa wake ambao alisema walikuwa bado wanatoka kuwahudumia waathiriwa.
"Hakuna maelezo bado, maafisa bado wako nje," Kimani aliambia Star.
Mabaki ya magari hayo mawili yalivutwa hadi kituo cha polisi cha KBC yakisubiri ukaguzi.
