Msemaji wa ikulu Kanze Dena amesema kwamba rais Uhuru Kenyatta hatafanikiwa kumaliza miradi yote ya ajenda nne kuu mwezi Agosti ambapo atakuwa anakamilisha kipindi chake cha uongozi.
Akifanya mahojiano na kituo kimoja cha habari nchini Jumanne, Kanze alisema kwamba baadhi ya miradi ipo ndani ya ruwaza ya 2030 na itakamilishwa na serikali inayofuata.
“Hata hivyo,serikali hii ya Jubilee imepiga hatua kubwa sana katika mpango wa ajenda nne kuu ikiwemo katika miradi ya uzalishaji, upatikanaji wa chakula miongoni mwa mingine,” Kanze alisema.
Kulingana naye, japo miradi mingi inaendelea kushughulikiwa, kumeshuhudiwa ufanisi mkubwa katika utekelezwaji wa miradi hiyo.
“Kuna miradi ya ujenzi wa nyumba inayoendelea kule Mtwapa na Buxton, miongoni mwa maeneo mengine,” alisema.
Aliongezea kwamba handshake kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ilisaidia kumaliza miradi mingi zaidi.
Kanze alisema kwamba rais Kenyatta anashirikiana na kaunti za eneo la Pwani ili kutoa hatimiliki 500,000 kwa wakazi wa eneo hilo.
Pia aliwataka wakazi kutafuta mbinu mbadala za kuzalisha chakula ili kutatua zogo la ukosefu wa chakula hasahasa katika vipindi vya kiangazi.
Alisema kuwa kufufuliwa kwa bandari ya Liwatoni kumechangia pakubwa ufanisi wa biashara ya bahari.