Sammy Ondimu Ngare, ni polisi msamaria mwema ambaye umaarufu wake ni kutokana na moyo wake wa kujitoa zaidi ya mipaka kuona binadamu wenzake wanafuraha kama wengine.
Afisa huyo wa polisi Alhamisi alichapisha simulizi ya kijana mmoja aliyeachwa na mamake zaidi ya miaka 10 iliyopita kutoka kaunti ya Kisii ambaye alishindwa kujiunga chuo kikuu kutokana na uhaba wa pesa.
Ngare alisema kijana huyo kwa jina Mosati Brian Areri amekuwa akisomeshwa na nyanya yake tangu kuachwa na mama yake akiwa shule ya msingi. Nyanya yake amemsimamia mpaka kumaliza kidato cha nne lakini pesa ya kukimu mahitaji yake ya chuo kikuu ndio ilikuwa mtihani.
“Mvulana huyo amekuwa chini ya uangalizi wa bibi yake ambaye pia ni mjane tangu akiwa mdogo hadi sasa, na bibi amejaribu kila awezalo kumwezesha kijana huyo kumaliza shule ya msingi na sekondari. Alipata alama za juu katika mitihani ya awali ya KCSE (🤓 lakini hakuweza kudahiliwa katika chuo kikuu cha MERU,” Ngare alisimulia.
Kufuatia madhira hayo, Ngare aliomba wahisani wema mitandaoni kumsaidia kupata japo shilingi elfu 30 pesa za Kenya ili kumlipia gharama ya kukubaliwa kujiunga chuo kikuu.
“Tafadhali wapendwa, ninashirikisha marafiki zangu wengi kumuona Mwana huyu kutoka kijijini kwangu ameenda shuleni. Bibi amefanya sehemu yake, hebu tuweke tabasamu kwenye uso wa kijana huyu. Mvulana huyu hawezi kumudu Ksh 28,600 na kwa njia hiyo yuko nyumbani bila msaada wowote. Tafadhali nahitaji marafiki 300 wanisaidie na 100 kila mmoja,” afisa Ngare aliomba.
Watu kadhaa walijitolea kwa moyo mkunjufu na kumsaidia kwa kutuma kidogo chochote kitu ili kumsaidia kijana huyo kuingia shule.
Kufikia asubuhi ya Ijumaa, Ngare alisema tayari alikuwa amepata zaidi ya shilingi laki moja kumwezesha kijana huyo kuingia chuoni na kuwashukuru wote ambao walizama mifukoni na kutrngana na kiasi cha pesa kwa ajili ya hilo.
“Nilikuwa nimeomba kusaidiwa na 30k karo ya shule chuo cha Meru lakini wakenya wamesaidia zaidi.. Wamefanya mara nne ya pesa nilizoomba. Tumefanikiwa Kuchangisha sh110,000. Na bado naona wakenya wanazidi kutuma. Mbarikiwe sana,” Ngare alishukuru kwa furaha.