logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Uhuru atimuliwa kama kiongozi wa chama cha Jubilee

Akitoa tangazo hilo, Kega alisema uamuzi huo ulitolewa na Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee

image
na

Yanayojiri02 May 2023 - 10:48

Muhtasari


  • Akitoa tangazo hilo, Kega alisema uamuzi huo ulitolewa na Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee wakati wa mkutano uliofanyika Jumanne.
Wakili Donald Kipkorir na rais Uhuru Kenyatta

Masaibu yanayoendelea katika chama cha Jubilee yamechukua mkondo mwingine baada ya mrengo unaomuunga mkono Rais William Ruto kumtimua Uhuru Kenyatta kama kiongozi wa chama hicho.

Timu hiyo inayoongozwa na kaimu katibu mkuu Kanini Kega amemteua mbunge mteule Sabina Chege kama kiongozi wa chama katika nafasi ya kukaimu.

Akitoa tangazo hilo, Kega alisema uamuzi huo ulitolewa na Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee wakati wa mkutano uliofanyika Jumanne.

"Afisi ya kiongozi wa chama kwa hivyo imetangazwa kuwa wazi na kusubiri uamuzi wa NDC Mhe. Sabina Chege atakuwa kaimu kiongozi wa chama cha Jubilee," Kega alisema wakati wa mkutano na wanahabari.

Kega alisema NEC ambayo alisema ilihudhuriwa na wajumbe 22 kati ya 28, ilifanya uamuzi baada ya Uhuru kudaiwa kukiuka katiba za chama na sheria za nchi.

Alitoa mfano wa Sheria ya Kustaafu na Mafao ya Rais ambayo inamzuia Uhuru kushika nafasi ya uongozi katika chama miezi sita baada ya uchaguzi.

Uhuru alipaswa kujiuzulu wadhifa wake wa chama kufikia Machi 13, ikiwa ni miezi sita baada ya kukabidhi mamlaka kwa Ruto.

“Kiongozi huyo wa zamani wa chama pia amejiendesha vibaya kwa kujidai kutoa matamshi kwa niaba ya chama,” alisema na kuongeza kuwa mwenendo wa Uhuru umetumwa kwa kamati ya nidhamu ya chama.

“Suala la utovu wa nidhamu linapelekwa kwenye kamati ya taifa ya nidhamu kwa hatua zaidi,” alisema.

Kwa mfano, Kega alisema Uhuru amekiuka katiba ya chama kwa kuitisha Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa Mei 22 kupitia maazimio ya NEC yaliyohudhuriwa na wajumbe saba pekee.

"Kikao cha NEC kilichodaiwa kuwa hakikuwa na akidi kama ilivyoainishwa na katiba, kilikuwa na wajumbe saba kati yao watatu wamesimamishwa kusubiri taratibu za utatuzi wa migogoro ya ndani," alisema.

Alisema kwa kufanya mkutano wa NEC na maafisa waliosimamishwa kazi, Uhuru alikuwa anakiuka katiba ya Jubilee.

Kwa mujibu wa timu ya Kega, notisi ya mkutano wa NEC haikutolewa ndani ya siku saba kama ilivyoainishwa kwenye katiba ya chama.

NEC ilisema hivi karibuni itachapisha notisi ya NDC ambapo wanachama wa chama hicho watapata fursa ya kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wa chama.

Uhuru wiki jana alivamia makao makuu ya Jubilee kwa nia ya kupigia muhuri mamlaka yake na kufutilia mbali mrengo wa Kega.

 

 

 

 

 

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved