logo

NOW ON AIR

Listen in Live

DCI watoa maelezo kuhusu wizi wa Eastleigh ulionaswa kwenye CCTV ambapo kijakazi alimsaidia jambazi

Kijakazi huyo wa Uganda aliyeajiriwa wiki tatu kabla ya tukio hilo pia alimsaidia jambazi kumvamia vibaya kijakazi mwenzake.

image
na Samuel Maina

Yanayojiri04 November 2024 - 08:24

Muhtasari


  • Mwizi liyekuwa amejihami kwa nyundo aliingia katika nyumba iliyo kwenye ghorofa ya 6 ya Ushirika Towers kwa usaidizi wa kijakazi ambaye anatoka Uganda.
  • Washukiwa hao wawili wanaripotiwa kufanikiwa kutoroka baada ya kutekeleza wizi huo.



Maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wanawasaka washukiwa wawili ambao wanaripotiwa kuhusika katika kisa cha hivi majuzi cha wizi katika jumba la Ushirika Towers, katika mtaa wa Eastleigh, jijini Nairobi.

Tukio hilo lilitokea Novemba 1, 2024 na lilinaswa kwenye CCTV. Video za tukio hilo zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku wanamtandao wengi wakitaka hatua ichukuliwe.

Katika taarifa yake Jumapili jioni, DCI ilithibitisha kwamba mvamizi aliyekuwa amejihami kwa nyundo aliingia katika nyumba iliyo kwenye ghorofa ya 6 ya Ushirika Towers kwa usaidizi wa kijakazi aliyetambulishwa kwa jina la Everlyne, ambaye anatoka Uganda.

Kijakazi huyo ambaye inasemekana alikuwa ameajiriwa katika nyumba hiyo takriban wiki tatu kabla ya tukio hilo pia anaripotiwa kumsaidia jambazi huyo kumvamia vibaya kijakazi mwenzake wa Kisomali mwenye umri wa miaka 20 kabla ya kuendelea kutekeleza wizi huo.

"Wakati wa tukio, vitu mbalimbali vya thamani viliibiwa, ikiwa ni pamoja na vipande vya vito vya dhahabu, kiasi kisichojulikana cha fedha za Kenya na dola za Marekani, pamoja na laptop nne za familia, ambazo ziliripotiwa kuibwa wakati wa tukio," DCI ilisema.

“Hakimo Muhidin alipata majeraha mabaya, ikiwa ni pamoja na kuvunjika jino na majeraha kwenye mkono, kichwa na miguu. Zaidi ya hayo, alionyesha dalili za kuchapwa, na alama zinazoonekana mgongoni mwake. Baada ya kupata matibabu, ameruhusiwa na kwa sasa anaendelea kupata nafuu katika nyumba ya jamaa,” taarifa hiyo ilizidi kusomeka.

Washukiwa hao wawili wanaripotiwa kufanikiwa kutoroka baada ya kutekeleza wizi huo.

Maafisa wa upelelezi wamefichua kuwa mmiliki wa nyumba hiyo alikuwa mbali na nyumbani pamoja na familia yake yote wakati kisa hicho kilipotokea.

"Mamlaka inaendelea na uchunguzi wao ili kupata maelezo zaidi kuhusu tukio hilo na waliko washukiwa," DCI ilisema.

Video za tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma na kuzua mjadala mkubwa na hisia tofauti kutoka kwa wanamtandao.


Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2026. All rights reserved