Watu sita ambao ni abiria waliokuwa kwenye basi wakitoka Mombasa wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya umma ya sultan Hamud kaunti ya Makueni.
Hii ni baada ya gari walimokuwa wakisafiria kugongwa na trela katika eneo la Mlima Kiu hatua chache kutoka soko la Salama Kaunti ya Makueni kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi usiku wa kuamukia leo.
Ripoti ya maafisa wa trafiki kutoka kaunti ndogo ya Mukaa zinasema ajali hii ilisababishwa na trela lilokuwa likotoka Nairobi wakati ambapo lilikuwa linapita magari mengine katika mteremko hatari wa Salama hivyo kugonga basi hilo upande mmoja na kupelekea ajali hii.
Majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya Sultan Hammud Level 4 ambapo walikuwa wamelazwa na kupokea matibabu.
Eneo la tukio lilihudhuriwa na kushughulikiwa na maafisa wa trafiki kutoka kituo cha polisi cha Mukaa.
"Trela lililokuwa likitoka Nairobi
kuelekea uelekeo wa jumla wa Mombasa lilikuwa likiyapita magari mengine kwenye
barabara kuu ya Nairobi - Mombasa eneo la Mlima Kiu wakati lilipogonga basi
lililokuwa likielekea kwenye kisa cha ajali," afisa wa polisi alisema.
Mabaki ya magari yote mawili yalivutwa hadi kituo cha polisi cha Salama yakisubiri ukaguzi.
Kisa hicho kilisababisha msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara kuu Jumapili asubuhi.