Maafisa wa upelelezi katika eneo la Masaba Kaskazini, kaunti ya Nyamira wanamzuilia mwanamume mmoja wa miaka 25 anayedaiwa kuhusika na makosa ya mitihani.
Kulingana na ripoti ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), mshukiwa Stephen Nyang'au Mbeche alikamatwa siku ya Jumapili, Novemba 10, na maafisa wa upelelezi wa Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) kwa ushirikiano na maafisa wa eneo la Masaba Kaskazini baada ya operesheni ya ufuatiliaji endelevu.
Imeripotiwa kuwa mshukiwa aliyekamatwa alikuwa msimamizi wa kundi la "KCSE 2024 Leakage Group" kwenye mtandao wa Telegram ambalo lilitumiwa kwa wizi wa mitihani.
"Upekuzi wa kina katika majengo yake ulisababisha kunaswa kwa simu ya rununu na kompyuta ndogo, vifaa vinavyodhaniwa kuwa anatumia kuwahadaa wazazi na wanafunzi waliohusika katika udanganyifu huo," ripoti ya DCI ilisoma.
Kurugenzi pia ilichapisha baadhi ya mazungumzo na karatasi zilizotumwa kwenye kikundi hicho cha Telegraph.
Mshukiwa huyo sasa anatayarishwa kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka mahakamani baada ya kukamatwa.
Anakabiliwa na mashtaka ya kumiliki vifaa vya mitihani visivyoidhinishwa, kinyume na sheria ya KNEC.
Idara ya DCI pia imetangaza kuwa msako mkali unaendelea ili kuwanasa washukiwa zaidi wanaohusika na makosa sawia.