Serikali ya kaunti ya Murang’a mnamo Jumatano jioni ilitangaza kifo cha MCA wa kuteuiwa, Mark G. Wainaina.
Wainaina alifariki hospitani alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa mbaya wa mapafu ambao ulikuwa umeathiri mapafu yake yote mawili.
Katika tangazo la kifo, gavana wa kaunti ya Murang’a Irungu Kang’ata alimuomboleza marehemu Mark kama kiongozi mchapakazi aliwayepigania watu haswa wenye matatizo ya kimwili.
"Serikali ya Kaunti ya Muranga yatangaza kupandishwa cheo hadi utukufu wa milele wa Mh Mark, Mwakilishi Mteule wa Bunge la Kaunti ya Muranga," Kang'ata alitangaza kupitia Facebook.
Aliongeza, "Mark alikuwa mwanachama mchapakazi ambaye alipigania haki za watu wake, haswa wale walio na uwezo tofauti. Tunaomba familia yake iwe na nguvu. Tutakosa kujitolea kwake.”
Marehemu Mark aliaga dunia siku chache kabla ya hafla ya kuchangisha pesa ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili yake katika juhudi za kutafuta pesa za bili ya hospitali.
Watu wenye nia njema walikuwa wamealikwa siku ya Ijumaa kwa chakula cha jioni cha kuchangisha pesa katika hoteli moja jijini Nairobi ili kusaidia kuchangisha pesa za matibabu ya MCA huyo wa kuteuliwa.
"Baraza la Wanachama wa Bunge la Kaunti ya Murang'a linakualika kwa karamu ya kuchangisha pesa ili kumsaidia mmoja wa mwanachama wetu Mhe Mark G. Wainaina ambaye amepatikana na ugonjwa mbaya wa mapafu ambao umefanya mapafu yake yote mawili kushindwa kufanya kazi," kadi iliyochapishwa na gavana Kang'ata mnamo Jumanne ilisomeka.
Hafla hiyo ilikuwa ifanyike katika Hoteli ya Sagret, mtaa wa Milimani, kaunti ya Nairobi kuanzia mwendo wa saa kumi na mbili jioni siku ya Ijumaa.