Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata na spika wa kaunti ya Kirinyaga Muteti Murimi hawakuweza kusoma jumbe za rambirambi za rais William Ruto na naibu wa rais Kithure Kindiki wakati wa mazishi ya marehemu MCA wa kuteuliwa Mark Gicheru Wainaina siku ya Jumamosi.
Ruto na Kindiki hawakuwepo katika mazishi hayo yaliyofanyika eneo la Kiharu lakini walikuwa wametuma jumbe zao kusomwa kwa waombolezaji wakati wa maziko hayo.
Kelele zilizoibuka kabla ya ujumbe wa naibu rais Kithure Kindiki kusomwa hata hivyo zilifanya hilo kutowezekana.
“Kwa watu wakuu wa Murang’a, waombolezaji wenzangu, mabibi na mabwana..” Spika Muteti alianza kusoma ujumbe wa Kindiki kabla ya waombolezaji kukatiza kwa kelele.
“Naomba mniruhusu nisome ili tumpe Mark heshima…” aliwasihi waombolezaji huku kelele zikiendelea.
Spika Muteti Murimi aliposhindwa kuendelea kusoma ujumbe huo, kasisi aliyekuwa anaongoza ibada ya mazishi aliingilia kati na kumtaka akabidhi ujumbe huo kwa familia ya marehemu Mark Wainaina.
Waombolezaji walisikika wakisherehekea na kupiga makofi huku spika wa kaunti ya Kirinyaga akienda kukabidhi karatasi kwa familia ya marehemu.
“Naomba tudumishe amani katika ibada hii, asanteni,” alisikika kasisi huyo huku gavana Irungu Kang’ata akisimama kuzungumza.
Gavana Kang’ata ambaye alikuwa akishikilia ujumbe wa rais William Ruto alisema kuwa angeukabidhi kwa familia badala ya kuusoma.
"Wacha pia niombe kwamba nikabidhi ujumbe wa rais kwa familia," alisema kabla ya kukabidhi karatasi hiyo kwa familia.
Haya yalijiri wakati wa mazishi ya marehemu MCA wa kuteuliwa wa kaunti ya Murang’a Mark Gicheru Wainaina yaliyofanyika Kirogo, eneo la Kiharu mnamo Jumamosi.
Wainaina alifariki mnamo Novemba 13 baada ya kuugua ugonjwa mbaya wa mapafu uliosababisha mapafu kushindwa kufanya kazi.