logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Omtata amjibu Atwoli kwa kudhalilisha azma yake kuwania urais

“Ajenda yetu imejikita katika utekelezaji kamili wa Katiba. Ni chombo chenye nguvu cha kuifanya nchi hii kuwa ya kisasa - Omtata.

image
na Davis Ojiambo

Yanayojiri28 November 2024 - 15:28

Muhtasari


  • Wakenya wa kawaida, sio mali au mapendeleo, ndio uti wa mgongo wa harakati zozote za kweli za mabadiliko," alisema.
  • Mawazo yetu yanawahusu wananchi, na tuna historia ya kusimama kidete kutetea kilicho sahihi,” alisema.
  • Atwoli alionyesha imani katika kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto mwaka 2027.



Seneta wa Busia Okiya Omtatah amemsuta Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli kufuatia maoni yake kuhusu azma yake ya urais. Atwoli siku ya Jumatano alikuwa amekosoa uwezo wa kifedha wa Seneta huyo, akimshauri kutathmini bajeti na rasilimali zake kabla ya kuwania urais.

"Iwapo angekuja kwangu, ningemwambia, 'Hebu nione bajeti yako. Je, utategemea watu wasamaria wema, au una nini kama mtu binafsi?'" Atwoli alisema.

"Unapogombea nafasi ya kisiasa, lazima uwe umeweka hifadhi ya kutosha. Ulimwenguni kote, hakuna mtu anataka kuhusishwa na mtu maskini." Akijibu madai ya Atwoli, Omtatah alisisitiza kwamba uongozi uko katika maono, uadilifu na kujitolea kuhudumu, na sio mali na mapendeleo.

"Wakenya wa kawaida, sio mali au mapendeleo, ndio uti wa mgongo wa harakati zozote za kweli za mabadiliko," alisema.

"Tutaonyesha kwamba kampeni inayoendeshwa na watu inaweza kuhamasisha matumaini na kutoa mustakabali mzuri kwa wote."

Mnamo Jumatano, Omtatah alizindua kamati yake ya kutahmini uwezo wake kuwania urais yenye wanachama 10, muda mfupi baada ya kutangaza nia yake ya kuwania kiti cha urais 2027. Alitanguliza utawala wa sheria na utekelezaji kamili wa Katiba ya 2010. Omtatah alisema maendeleo ya nchi yamezuiwa na ukosefu wa nia ya kisiasa ya kutekeleza vipengee vya kikatiba.



Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli mwenye kipaza sauti


“Ajenda yetu imejikita katika utekelezaji kamili wa Katiba. Ni chombo chenye nguvu cha kuifanya nchi hii kuwa ya kisasa,” alisema.

"Sura mahususi, haswa kuhusu fedha za umma, hutoa mwongozo wazi, lakini utashi wa kisiasa umekosekana, na kufanya Katiba ionekane kuwa haina nguvu."

Alisisitiza umuhimu wa kampeni inayoendeshwa na watu, akiongeza kuwa haitategemea rasilimali nyingi za kifedha badala yake itazingatia kuwashirikisha Wakenya katika mijadala yenye maana. "Hatuna pesa za kuchoma, lakini tuna mawazo na mpango thabiti.

Mawazo yetu yanawahusu wananchi, na tuna historia ya kusimama kidete kutetea kilicho sahihi,” alisema.

Kwa upande wake Atwoli alisema Seneta Omutata anafaa kuzingatia ushirikiano na viongozi wa kanda na kuhakikisha kuwa yuko tayari kifedha kabla ya uchaguzi wa 2027.

"Lazima Okiyah aulete uongozi wa Magharibi pamoja," Atwoli alisema.

"Lazima awasiliane na watu kama Amos Wako, aende Bungoma na kushauriana na watu kama Moses Wetang'ula, na atafute (mkuu wa Waziri Musalia). Akitoka hapo afanye mkutano wa pamoja na tutaweza kumweleza iwapo ataweza au la,” alisema.

Atwoli alionyesha imani katika kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto mwaka 2027.

"saa  nne asubuhi 2027," Atwoli alisema.

Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved