logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Atwoli aibua madai ya baadhi ya Wakenya kujiteka nyara ili kupata ufadhili

"Haki yako sio muhimu kuhujumu haki za wengine. Ni lazima tuheshimu afisi ya Rais,” Atwoli alisema.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri03 January 2025 - 14:46

Muhtasari


  • Atwoli alisema anafahamu visa kama hivyo kutokana na mahusiano yake makubwa na mashirika yanayovuka mipaka.
  •  Atwoli alisema wazazi lazima wawafundishe watoto kuwa watu wenye heshima, ambao hawafai kutumia mitandao kwa njia mbaya.

Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli amedai kwamba baadhi ya watu nchini hujiteka nyara ili kupata ufadhili kutoka kwa mashirika ya hisani.

 Akizungumza wakati wa mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula, Atwoli alisema anafahamu visa kama hivyo kutokana na mahusiano yake makubwa na mashirika yanayovuka mipaka.

 “Kwenye utekaji nafanya kazi na mashirika mengi duniani, baadhi ya watu wanajiteka ili wapate fedha kutoka kwa baadhi ya mashirika,” alisema.

 Atwoli aliongeza kuwa wazazi lazima wawafundishe watoto wao kuwa watu wenye heshima, ambao hawafai kutumia mitandao ya kijamii kwa njia mbaya.

 "Haki yako sio muhimu kuhujumu haki za wengine. Ni lazima tuheshimu afisi ya Rais,” alisema.

 Atwoli alikuwa akizungumza Ijumaa katika ibada ya mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula na Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi.

 Rais William Ruto, Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, Wabunge kadhaa, Magavana, Mawaziri na maafisa wengine wa serikali walihudhuria.

 Wengi wa waliotoa hotuba walizungumzia utekaji nyara huku washirika wa Ruto walipohamia kutetea serikali dhidi ya chuki hizo.

 Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya hata hivyo alitofautiana na Atwoli kuhusu suala la utekaji nyara.

 “Nasema hivi kwa moyo mzito sana. Kwa kiongozi kusimama hapa na kusema watu wanajiteka na kujiua ni bahati mbaya. Sio kwa misingi hii takatifu,” aliongeza.

 “Watoto wetu wanapotea na kuuawa; huo ndio msimamo.”

 Matamshi hayo kuhusu utekaji nyara yanajiri wakati wakenya wakidai majibu kuhusu waliko Wakenya kadhaa waliochukuliwa na watu wasiojulikana katika maeneo tofauti nchini.

 Baadhi ya wathiriwa wanaodaiwa kutekwa nyara bado hawajulikani waliko.

 Mnamo Jumatatu, baadhi ya Wakenya walifanya maandamano ya kutaka kuachiliwa kwa kundi hilo lakini hakuna hata mmoja wao aliyeachiliwa.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved