logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kuria awakashifu waombolezaji waliokataa ujumbe wa Ruto kusomwa katika mazishi ya mwanawe Kivuti

Kuria amemtaka Bw Kivuti, ambaye mwanawe alikuwa akizikwa, kujitenga na kile kilichotokea.

image
na Samuel Maina

Yanayojiri04 January 2025 - 11:48

Muhtasari


  • Kuria amekashifu kisa ambapo waombolezaji walizuia kusomwa kwa ujumbe wa rambirambi wa Rais Ruto wakati wa mazishi ya mwanawe Lenny Kivuti.
  • Kuria alibainisha kuwa kukataa rambirambi ni kinyume na utamaduni wa jamii yao.


Mshauri Mkuu katika Baraza la Washauri wa Uchumi wa Ikulu Moses Kuria amekashifu kisa ambapo waombolezaji walizuia kusomwa kwa ujumbe wa rambirambi wa Rais William Ruto wakati wa mazishi ya mwanawe mwanasiasa Lenny Kivuti.

 Rais Ruto alikuwa ametuma ujumbe usomwe kwa familia na waombolezaji wakati wa mazishi hayo yaliyofanyika Embu siku ya Ijumaa lakini waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi hakuweza kusoma ujumbe huo kufuatia kelele kutoka kwa waombolezaji ambao hawakutaka kusikia kilichokuwa kimeandikwa.

 Akizungumzia tukio hilo katika taarifa yake Jumamosi asubuhi, Kuria alibainisha kuwa kukataa rambirambi ni kinyume na utamaduni wa jamii yao.

"Katika Utamaduni Wetu, KAMWE hatukatai rambirambi hata kutoka kwa maadui zetu wakubwa. Jumbe husomwa hadharani kwa ajili ya faraja ya familia iliyofiwa. Ndiyo sababu maombi hufanywa hadharani ikiwa ni pamoja na maombi kwa ajili ya familia (Vinginevyo makasisi wangerudi nyuma ya hema na familia na kuomba faraghani,” Kuria alisema.

Waziri huyo wa zamani wa Utumishi wa Umma aliendelea kumtaka Bw Kivuti, ambaye mwanawe alikuwa akizikwa, kujitenga na kile kilichotokea.

“Natarajia Sen Leny Kivuti kujitenga na kitendo hiki kisicho cha kimungu. Sio lazima umpende Rais bali ni HAKI yake kufariji familia,” alisema.

Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi alishindwa kusoma ujumbe wa rambirambi wa Rais William Ruto wakati wa mazishi ya mwanawe aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti, Eric Kivuti siku ya Ijumaa.

 Rais hakuweza kuhudhuria ibada hiyo kwa kuwa alikuwa katika mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula huko Bungoma.

Hata hivyo, alikuwa ameandika ujumbe wa kusomwa kwa familia na waombolezaji.

Wakati Waziri Muturi aliposimama kusoma ujumbe huo, umati ulianza kupiga kelele, hivyo ikawa vigumu kwake kuendelea. "Nimepewa ujumbe wa rambirambi, kutoka kwa Mheshimiwa Rais... (kelele) Sasa pale nimefika mwisho ni kwamba nimepewa ujumbe. Niwapatie. Nisome ama nisisome?" Muturi aliuliza

 Umati ulijibu kwa kusema "Usisome".

Waziri alionekana akimshirikisha Askofu aliyekuwa akiongoza ibada kabla ya kuendelea. 

 "Nimeshauriwa kwa busara na unajua kama spika wa zamani… na mnajua marehemu JJ Kamotho, aliwahi kusema kuhusu kura ya makelele, nimeskia kura ya makelele.... Niko na heshima kufikisha ujumbe huu kwa Mhe lenny Kivuti hadharani,” alisema.

 Muturi alikiri jibu lao, akieleza kuwa alikuwa ameshauriwa kusoma ujumbe huo hadharani.


Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2026. All rights reserved