logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Utata huku mwili wa mwanaharakati kijana aliyetoweka ukipatikana Thika

Mwili wa Ibrahim Mwiti ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Thika Level Five.

image
na Samuel Maina

Yanayojiri04 January 2025 - 08:16

Muhtasari


  • Mwili wa Mwiti  ulipatikana zaidi ya mwezi mmoja baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoweka katika mazingira yasiyoeleweka.
  • Mwiti alionekana mara ya mwisho katikati mwa jiji la Nairobi kabla ya kutoweka, jambo lililosababisha msako wa familia yake.

8541b3ed-1728-4ea5-ba3b-41ed24b018aa.png (461×521)

Mwili wa mwanaharakati Ibrahim Hilal Mwiti ambaye alitoweka Novemba mwaka jana ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Thika Level Five.

 Hii ilikuwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoweka katika mazingira yasiyoeleweka.

 Polisi na maafisa wa chumba cha kuhifadhia maiti walisema kifo hicho kilitokana na kugongwa na gari ambalo lilitoroka eneo la tukio.

 Mwiti alionekana mara ya mwisho katikati mwa jiji la Nairobi kabla ya kutoweka, jambo lililosababisha msako wa familia yake.

 Marafiki zake walizamia kwenye mitandao ya kijamii kutafuta usaidizi wa kumpata.

 Familia ilisema iliwasilisha taarifa ya mtu aliyepotea katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji mnamo Novemba 15, 2024, chini ya OB nambari 80A/13/11/24.

 Msako wao uliishia kwa kilio baada ya kutambua mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti mjini Thika mnamo Januari 2, 2025.

 Mwiti alijipatia riziki kama mtu wa kusambaza mizigo umbali wa kilomita 45 kutoka mahali alipoonekana mara ya mwisho.

 Mazingira kuhusu kifo cha Mwiti bado hayaeleweki.

 Mamake, Sadhiya Iman alisema walikuwa wamemtafuta Mwiti karibu kila mahali kabla ya kufanya uamuzi mchungu wa kutembelea vyumba vya kuhifadhia maiti jijini Nairobi na viunga vyake, hatua ambayo hatimaye iliwafikisha katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Thika Level Five.

 "Tulifahamishwa kwamba kesi yake ilikuwa tukio la kugongwa na kukimbia. Hatujui chochote kuhusu kifo chake," alisema.

 "Tunataka kujua hali ya kifo cha mwanangu."

 Pia alifichua kuwa kabla ya kifo chake, Mwiti alikuwa amepoteza kitambulisho chake na alipata taabu sana kupata kingine.

 Hili lilifanya maisha yake kuwa magumu kwa sababu alikuwa akiombwa kujitambulisha kila anapohitaji huduma ya serikali au kuzuiwa na polisi.

 Marafiki zake walisema hawaamini kuwa ilikuwa ni tukio la kugongwa na gari. Polisi bado hawajatoa tamko kuhusu kesi ya Mwiti.

 Haya yanajiri wakati ambapo Wakenya wamezua wasiwasi mwingi na kutaka majibu kuhusu visa vilivyokithiri vya utekaji nyara na watu kutoweka kwa njia ya kutatanisha.

 Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, visa vya utekaji nyara na kutoweka kwa watu kwa nguvu vimekuwa vya kawaida huku wazazi wakiishi kwa hofu ya vijana wao kutoweka bila kujulikana.

 Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, kumekuwa na takriban visa 82 vya utekaji nyara tangu Juni 2024, kipindi ambacho vijana walijitokeza barabarani kupinga Mswada wa Fedha.

 Katika miezi mitatu iliyopita ya 2024, angalau visa 13 vya utekaji nyara vilirekodiwa huku Desemba pekee ikichukua saba, Tume ilisema.


Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2026. All rights reserved