Tanzania imethibitisha kisa cha pili cha ugonjwa wa Marburg, na Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) inasema serikali inatarajiwa kuomba dawa na chanjo.
“Tuna imani na matokeo kutoka Tanzania,” alisema Dkt. Ngashi Ngongo, Mkuu wa Africa CDC, alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kila wiki.
Vifo tisa vilivyodhaniwa kuwa vya Marburg vimekuwa vikifanyiwa uchunguzi, huku moja pekee ikithibitishwa alifariki kutokana na ugonjwa wa Marburg.
Serikali ya Tanzania imetoa tahadhari ya kusafiri kwa abiria kutoka Kagera, na inachunguza watu waliokutana na wagonjwa na hawaruhusiwi kuondoka katika maeneo yao ya kujitenga hadi wahakikishwe na mamlaka za usafiri.
Mamlaka ya kudhibiti na kuzuia Magonjwa Afrika CDC pia inajiandaa kutuma timu za maandalizi katika nchi za Afrika Mashariki.
Wakati huo huo Kenya iko katika tahadhari kubwa. Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Kenya, nchi hiyo imetengwa kama nchi iliyo katika hatari kubwa ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg, hasa kwa sababu ya mkoa wa Kagera kuwa ni kituo cha usafirishaji katika eneo hilo, na watu wengi kusafiri kwenda na kurudi kutoka Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Shirika la Afya duniani WHO limetoa msaada wa dola milioni 3 kwa Tanzania, huku Africa CDC ikisaidia kupata ufadhili zaidi kwa ajili ya mpango wa kukabiliana na ugonjwa wa Marburg wa dola milioni 10.


