Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya sasa anasema kwamba swala la kuwapa vitambulisho watu wa mashariki mwa Kenya pasipo kupigwa msasa kutaongeza madhara.
Natembeya anasema kwamba mpango huo wa serikali huenda ukaeka nchi matatani kwa masaibu ambayo itakua vigumu kuyaondoa.
Natembeya alionya kuwa mabadiliko ya sera ya Ruto yanaweza kuruhusu watu kutoka makundi ya kigaidi yaliyopigwa marufuku kuingia nchini, kupata hati za utambulisho, na kuna uwezekano hata wa kupenya nafasi za uchaguzi siku zijazo.
"Jambo hili lina maana kubwa ya usalama, hili si jambo la kufanya kwa namna yoyote kwani itafikia hatua kwamba hata MCA atachaguliwa kutoka kwa vikundi vilivyopigwa marufuku nchini. Tutakuwa na matokeo ya hatari zaidi wakati hata Gavana, Mbunge, au hata Rais atachaguliwa kutoka kwa vikundi hivyo," aliongeza Natembeya.
Gavana huyo ambaye ni mtaalamu wa zamani wa usalama na msimamizi wa eneo la Rift Valley, alisisitiza kuwa agizo hilo halikushauriwa vizuri na litakuwa na athari kubwa za kidiplomasia.
"Sisi kama watu ambao tuko katika nyadhifa ya serikali, tunatakikana tumushauri rais vizuri sana kwa sababu itafika mahali tukipeana sitakabadhi zetu kiholela, sitakabadhi ambazo zinaheshimiwa sana, itafika mahali pia tuanze kudharauliwa. tutaanza kufanyiwa uchunguzi wa ziada wakati mtu anasafiri."
Wakati huo amewataka wakenya kuelewa kwamba maneno yake hayatokani na uhasama wa siasa bali hilo jambo la rais lafaa kujadiliwa kwa umakini sana.
Amesitiza kwamba kufungua mipaka kwa watu kupewa vitambulisho bila kufanyiwa uchunguzi kuna athari zaidi kuliko faida kwa wakenya na litaletea taifa mchanganyiko.
"Itakuwa ni Scramble for Kenya. wanafunguwa shida ambayo hawataweza kuifunga. Mimi mwanzo nimeshaogopa kabisa kwamba unakuja hapa umebeba kitambulisho na wewe ni gaidi na hakuna mtu anayefahamu historia yako kukuhusu unakuja tu na unapewa kitambulisho," George Natembea alieleza.
Gavana huyo, anayejulikana kwa msimamo wake thabiti juu ya sera za serikali, pia ameonya zaidi kwamba maagizo hayo yanaweza kuruhusu wahalifu kuingilia usalama wa nchi ya Kenya na utovu wa nidhamu.
"Wale waliowateka machifu wetu watapewa vitambulisho vya taifa la Kenya. Kwa hivyo wakiendelea na mazoezi yao ya utekaji nyara, watabeba vitambulisho,'' Natembea alibainisha
"Baadhi yao hata watapenyeza ndani ya vyombo vya usalama wa nchi yetu ikiwa ni pamoja na polisi, jeshi au hata timu ya kusindikiza ya Rais itakuwa na kamanda wake kuwa mhalifu."
Akilinganisha na maagizo ya kiutendaji yaliyotiwa saini na Rais wa Marekani Donald Trump, Natembeya alisema kuwa Ruto alipaswa kuchukua hatua kama hiyo katika kushughulikia masuala ya usalama wa taifa.