Seneta wa Kaunti ya Baringo, William Cheptumo, amefariki dunia.
Cheptumo aliaga dunia akiwa katika Hospitali ya Nairobi, ambako alikuwa akipokea matibabu kwa ugonjwa ambao haukuwa wazi kwa umma.
Kwa mujibu wa familia yake, marehemu alikuwa akiugua kwa muda mrefu hadi kufariki tarehe 16 Februari.
Mmoja wa famili yake alifichua kuwa wiki iliyopita aliruhusiwa kutoka hospitalini, lakini hali yake ilidhoofika tena, jambo lililomfanya arudishwe hospitalini.
Rais William Ruto aliongoza taifa katika kuomboleza kifo chake, akimtaja kama kiongozi mwenye maono na aliyejitolea kwa maslahi ya wananchi.
"Cheptumo alikuwa mzalendo, mchapakazi na mtetezi wa maendeleo ya Baringo. Tunawapa pole familia yake, marafiki na wakaazi wa Kaunti ya Baringo," Rais aliandika kupitia mtandao wa X.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hifadhi ya wafu ya Lee Funeral Home.
Marehemu Cheptumo, aliyekuwa na umri wa miaka 57, alikuwa wakili kwa taaluma na alihudumu kama Mbunge wa Baringo Kaskazini kati ya mwaka 2008 na 2013.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, alichaguliwa kuwa Seneta wa Baringo kupitia chama cha UDA, akimshinda Gideon Moi wa KANU.
Alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa, Ulinzi na Masuala ya Kigeni katika Seneti.
Cheptumo pia alikuwa mwanzilishi wa kampuni ya uwakili ya Cheptumo and Company Advocates.
Kabla ya kujitosa kwenye siasa, alifanya kazi kama afisa wa sheria katika Benki Kuu ya Kenya na Shirika la Maendeleo ya Viwanda na Biashara (ICDC).