KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Jumatatu, Februari 17.
Katika taarifa ya Jumapili jioni, kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanyika kwenye mitambo.
Walisema baadhi ya maeneo ya kaunti sita za Kenya yatakosa umeme kati ya saa mbili unusu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na Bomet, West Pokot, Nandi, Nyeri, Murang'a, na Kiambu.
Katika kaunti ya Bomet, sehemu za maeneo ya Sotik na Chepilat zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Sehemu za maeneo ya Makutano na Lelan katika kaunti ya West Pokot zitakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Maeneo ya Kamobo na Kapsasur katika kaunti ya Nandi pia yataathirika kati ya saa tatu unusu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Katika kaunti ya Nyeri, sehemu za maeneo ya Ihwagi Market, na Ragati Tea Factory zitakosa stima kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Maeneo ya eneo la Ikumbi katika kaunti ya Murang'a yataathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Wakati huohuo, sehemu za maeneo ya Kiganjo na Athena Primary katika kaunti ya Kiambu pia zitakosa umeme.