Seneta wa Busia na mwanaharakati mashuhuri Okiya Omtatah ameikosoa vikali Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na Idara ya Ujasusi ya Kitaifa (NIS) kwa kuhusika katika siasa za ndani, akisema hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa Katiba.
Kauli ya Omtatah imejiri siku moja baada ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Charles Kahariri, na Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Ujasusi (NIS), Noordin Haji, kutoa matamshi makali kuhusu kampeni ya "#RutoMustGo" wakati wa mhadhara wa kitaaluma ulioandaliwa katika Chuo cha Kitaifa cha Utafiti wa Ujasusi (NIRU).
Katika hotuba yao, viongozi hao wa usalama waliashiria kuwa kampeni hiyo inaweza kuhatarisha utulivu wa taifa, huku Jenerali Kahariri akisisitiza kuwa jeshi halitaruhusu "uasi wa kikatiba."
"Hatuwezi kuwa na vurugu kama taifa. Watu wanapofanya maamuzi yao kidemokrasia, lazima wajue kuwa mabadiliko ya serikali ni kwa njia za kikatiba," alisema Kahariri, akihimiza Wakenya kutegemea kura badala ya maandamano katika kushinikiza mabadiliko ya uongozi.
Hata hivyo, Omtatah ameeleza kusikitishwa na matamshi hayo, akisema kwamba taasisi za usalama zinapaswa kusalia huru na kutokuwa na upande wowote wa kisiasa.
Akirejelea Ibara ya 239(3) ya Katiba, alikumbusha kuwa vyombo vya usalama haviruhusiwi kushiriki katika siasa kwa njia yoyote. Alisisitiza kuwa kauli zilizotolewa na KDF na NIS kuhusu kampeni ya "#RutoMustGo" zinakiuka katiba kwa kupendelea upande mmoja wa kisiasa.
"KDF imeundwa chini ya Ibara ya 241(2)(a) ya Katiba ili kutetea na kulinda uhuru na mipaka ya nchi. Hakuna popote wanaruhusiwa kuingilia masuala ya siasa za ndani," alisema Omtatah, akiongeza kuwa jeshi linafaa kushughulika na ulinzi wa taifa badala ya kujihusisha na mijadala ya kisiasa.
Katika hotuba yake, Jenerali Kahariri alizungumzia hali ya usalama katika eneo la Afrika Mashariki, akitaja vita vya Sudan, mapigano yanayoendelea Ethiopia, na changamoto za kiusalama katika Sudan Kusini kama sababu zinazofanya KDF kuwa macho zaidi.
Lakini kwa mujibu wa Omtatah, kauli hizo zilionekana kuwa na ajenda fiche ya kuhalalisha uwepo wa jeshi katika masuala ya ndani ya Kenya.
Omtatah ameitaka serikali kueleza wazi msimamo wake kuhusu nafasi ya vyombo vya usalama katika siasa za kitaifa. Alisema ni muhimu kwa Mkurugenzi Mkuu wa NIS na Mkuu wa Majeshi kutoa tamko rasmi la kuthibitisha msimamo wao wa kutopendelea upande wowote kisiasa.
Aidha, ametoa wito kwa Bunge kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai ya matumizi mabaya ya taasisi za usalama kwa faida za kisiasa, akisema kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya kuvunja katiba anapaswa kuwajibishwa kisheria.
"Hatuwezi kuruhusu taasisi za usalama kutumiwa kama silaha za kisiasa. Hili likiachwa, historia inatuonyesha kuwa linaweza kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu na mkwamo wa maendeleo," alionya Omtatah.
Mvutano huu unakuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la
shinikizo la wananchi, hasa vijana wa kizazi cha Gen Z, wanaotaka mabadiliko ya
uongozi. Swali linalosalia ni iwapo serikali itajibu madai haya au kuendelea na
msimamo wake wa sasa.