
Shirika la Kenya Power limeungana na sekta ya nishati ya Afrika Mashariki kuomboleza kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Eng. Gissima Nyamo-Hanga, aliyeaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani usiku wa kuamkia Jumapili, Aprili 13, katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara, Tanzania.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumatatu asubuhi, Kenya Power imemtaja marehemu kama kiongozi mwenye maono, ambaye alijitolea kwa dhati kusukuma mbele ajenda ya ushirikiano wa nishati katika ukanda huu.
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa sekta ya nishati katika ukanda huu na kimegusa kwa kina TANESCO na uongozi mzima wa Kenya Power,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwananchi, ajali hiyo ilitokea baada ya gari la marehemu kugongana uso kwa uso na lori, wakati akijaribu kumuepuka mwendesha baiskeli. Eng. Nyamo-Hanga na dereva wake walifariki dunia papo hapo.
Marehemu aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO mwezi Septemba 2023, baada ya kuhudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, alisukuma mbele ushirikiano muhimu kati ya Kenya na Tanzania katika sekta ya nishati.
“Katika miezi ya hivi karibuni, aliongoza kwa mafanikio timu
ya TANESCO katika mazungumzo ya Mkataba wa Kubadilishana Nishati na Kenya
Power, jambo lililowezesha uzinduzi na uanzishaji rasmi wa njia ya umeme ya
msongo wa kV 400 kati ya Kenya na Tanzania, ambayo sasa inatumika kikamilifu
kwa biashara ya umeme mipakani,” ilieleza taarifa ya KPLC.
Kenya Power pia ilimpongeza kwa mchango wake katika Kamati ya Uongozi ya East African Power Pool (EAPP), ambapo alihusika katika kuandaa mazingira ya biashara ya nishati kwa nchi wanachama 13 wa ukanda huu.
“Atakumbukwa kama mjumbe aliyejitolea kwa dhati katika Kamati ya EAPP, akichangia kuweka misingi ya biashara ya umeme ya baadaye katika Afrika Mashariki,” iliongeza Kenya Power.
Taarifa ya Kenya Power ilihitimishwa kwa kutoa rambirambi na heshima kwa maisha na mchango wa marehemu:
“Tunamheshimu kwa urithi alioacha na tunatoa pole zetu za dhati kwa familia yake, uongozi wa TANESCO, wenzake na jamii nzima ya sekta ya nishati,” ilisema Kenya Power.
Kifo cha Eng. Nyamo-Hanga kimetokea wakati ambapo ukanda wa Afrika Mashariki unapiga hatua katika ushirikiano wa nishati.
Wataalamu wanasema mchango wake utabaki kuwa wa thamani kwa kizazi cha sasa na kijacho.