Rais Uhuru Kenyatta ameomboleza kifo cha aliyekuwa mbunge wa Kuria Mashariki Shadrack Roger Mwita Manga aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa na mwanahabari marehemu Lorna Irungu aliyefariki Jumatatu, akisema Kenya imepoteza viongozi wenye maono ambao walikuwa mfano mwema wa huduma kwa taifa.
Katika ujumbe wake kwa familia, jamaa na marafiki wa marehemu Mbunge Shadrack Manga, Rais Kenyatta alisema, Kenya na haswa wakaazi wa Kuria watathamini milele mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya eneo hilo.
Rais alisema marehemu Manga alikuwa shupavu katika mijadala bungeni huku hoja zake zikichangia pakubwa sana ajenda ya sheria ya Kenya na usimamizi wa bunge.
Rais alisema marehemu mbunge huyo alijitambulisha kama msimamizi wa kutegemewa na mtetezi wa masilahi ya umma kwa kupigania sheria bora kuwawezesha Wakenya kuboresha maisha yao.
“Nakumbuka kujitolea na kujituma kwake katika kuweka mazingira bora kwa watu wetu kushiriki katika maendeleo ya uchumi wakati alikuwa mwanachama wa Kamati ya Bunge ya Fedha, Mipango na Biashara. Hakika, alikuwa mtumishi wa umma aliye na umakini na aliyejitolea ambaye atakumbukwa kwa ushauri wake wa busara na uongozi thabiti, "Rais Kenyatta alisema.
"Tumepoteza kiongozi shujaa ambaye mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa nchi utakumbukwa kwa vizazi vijavyo," Rais alimsifu Manga.
Rais alimwomba Mungu ampe mkewe Anne Wesiko Manga na familia nzima ya marehemu nguvu na ujasiri wa kuhimili kifo chake.
Wakati huo huo rais Kenyatta pia alituma risala za rambi rambi kwa familia, marafiki na jamaa wa marehemu Lorna Irungu, Rais alimtaja kama raia bora ambaye alitumia talanta na ushawishi wake kuendeleza masilahi ya kitaifa.
Alisema kuwa kama mwandishi wa habari hodari na mjuzi, Lorna alitumia taaluma yake katika tasnia ya burudani kutengeneza nafasi kwa wasanii wa Kenya katika sanaa ya maonyesho na alifanya kazi bila kuchoka kukuza sauti za wanawake katika vyombo vya habari na uongozi.
Kiongozi wa taifa alikumbuka Lorna kwa juhudi zake katika kuwafanya vijana kusajiliwa kupiga kura, kuwashirikisha wanawake kote nchini kupitisha katiba ya Kenya ya 2010, na utetezi uliosababisha kupitishwa kwa Muswada wa Makosa ya Kijinsia mnamo mwaka 2006.
"Nimemfahamu Lorna kwa miaka mingi na nilipenda roho yake ya kupigana licha ya changamoto za kiafya alizokumbana nazo. Yeye ni msukumo kwetu sote tusikate tamaa wakati mambo yatakuwa magumu, ”Rais alisifu.
Rais Kenyatta alimwomba Mungu ampe faraja mumewe Edwin Macharia na binti yake Nancy Mumbi Macharia, pamoja na familia yao kubwa wakati huu mgumu wa maombolezo.