Msichana mmoja wa miaka 16 aliponea kifo chupuchupu baada ya jaribio la kuavya mimba kuenda vibaya wikendi iliyopita.
Mwanafunzi huyo wa darasa la nane anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Kitui baada ya kujifungua kijusi cha kiume cha miezi 5 kisicho hai katika kituo cha afya cha Mumoni ambako alikimbizwa kufuatia maumivu.
Kulingana na kitengo cha DCI, mama ya mhasiriwa alisema bintiye alianza kulalamika kuhusu maumivu ya tumbo na ndiposa akamkimbiza hospitalini.
Baada ya kuhojiwa msichana huyo alifichua kuwa mwalimu mkuu wa shule yao, ambaye ndiye mwenye kumpachika ujauzito alimpeleka katika hospitali ndogo ya kibinafi katika maeneo ya Ishiara siku ya Jumamosi ambapo alipatiwa vidonge na kuagizwa ameze.
Baadae baada ya kumeza vidonge hivyo mhasiriwa alianza kuumwa na tumbo na kulazimu apelekwe hospitali.
Shughuli ya kumsaka mshukiwa ambaye kwa sasa ameingia mitini pamoja na mmiliki wa hospitali iliyotekeleza mimba imeanzishwa.
