Waziri wa michezo, sanaa na maswala ya vijana Kipchumba Murkomen, mnamo Alhamisi asubuhi amezindua bodi mpya ya Sports Kenya.
Sports Kenya na ni shirika la serikali ambalo linasimamia vifaa vya michezo ikiwemo viwanja, kuendesha programu za michezo pamoja na kukuza utalii wa michezo nchini.
Kuzinduliwa kwa bodi hiyo kunajiri wakati Kenya inajiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN yatakayoandaliwa klwa ushirikiano na mataifa ya Tanzania na Uganda. Vile vile, nchi hizo tatu za Afrika Mashariki zinatarajia kuandaa kipute cha AFCON cha mwaka 2027, ambapo Kenya ipo mbioni kukarabati viwanja vitakavyotumika katika michuano hiyo.
Bodi iliyoasisiwa inatarajiwa kuhakikisha viwanja hivyo vinakuwa tayari kuandaa CHAN ya mwakani. Waziri Murkomen amesema kuwa kupitia bodi hiyo, serikali lazima imalize ukarabati wa viwanja kwa muda unaostahili, kuimarisha ubora wa viwanja hivyo na kuhakikisha vinalindwa kupitia uongozi ulio bora.
Bodi
hiyo inayoongozwa na mwenyekiti Mark Lomunokol, ina wanachama wageni ambao ni
William Odaji, Mohamed Shoaib Vayani na Richard Kimutai Chemweno.
Wanachama hao wapya walifanya ziara ya kufahamu
miradi ya shirika la Sports Kenya katika jiji la Nairobi. Wakiwa pamoja na
waziri Murkomen Alhamisi, walizuru uwanja wa Kasarani na Nyayo unaofanyiwa
ukarabati pamoja na uwanja mpya unaojengwa wa Talanta Sports City.

© Radio Jambo 2024. All rights reserved