
Kibera Soccer Women FC ndiyo mabingwa wapya wa Kombe la Wanawake la Shirikisho la Soka Kenya (FKF) baada ya kuifunga Vihiga Queens 1-0 katika mechi kali iliyopigwa leo kwenye Uwanja wa Afraha, Nakuru.
Mchezaji wa akiba, Stellah Odhiambo, aliipatia Kibera bao la ushindi katika dakika ya 90 baada ya kumalizia krosi murua kutoka kwa Yvonne Idagiza, na kuwafanya benchi na mashabiki wa Kibera kusherehekea kwa shangwe kubwa.

Katika kipindi cha kwanza, Kibera walikaribia kuongoza dakika ya 14 kupitia Faith Mboya, lakini shuti lake kali liligonga mwamba wa juu wa goli, na kipindi cha kwanza kikamalizika bila mabao.
Juhudi za mwisho za Vihiga Queens kusawazisha hazikufua dafu, huku Kibera wakidhibiti mchezo kwa mashambulizi ya mara kwa mara hadi filimbi ya mwisho, na kuibuka na ushindi wa 1-0.
Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Kibera, David Busego, aliisifu timu yake kwa kudhihirisha ujasirI katika fainali hiyo.
“Ninajivunia sana wasichana wangu. Ilikuwa mechi ngumu. Tulikosa nafasi nyingi kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili tulirekebisha makosa yetu, tukaongeza mashambulizi, na tukapata matokeo.”
Kwa upande wake, kocha wa Vihiga Queens, Boniface Nyamunyamu, alikiri kuwa kupoteza umakini kwa muda mfupi kuliwagharimu.
Alisema, “Tulipoteza umakini dakika ya mwisho, na hilo likatuadhibu. Hata hivyo, ilikuwa mechi nzuri, timu zote zilicheza vyema. Tutarudi kufanya tathmini ya makosa yetu na kurudi tukiwa na nguvu msimu ujao.”
Faith Mboya wa Kibera alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP), huku Diana Cheron wa Vihiga Queens akiibuka na Kiatu cha Dhahabu.
Kipa wa Vihiga, Vivian Khayati, alitunukiwa tuzo ya Kipa Bora.
Kibera Soccer walizawadiwa Shilingi 650,000, huku Vihiga Queens wakipokea Shilingi 100,000.