
Kocha mkuu wa Tusker FC, Charles Okere, amesema atapa kipaumbele usajili wa washambuliaji huku timu hiyo ikijiandaa kwa msimu mpya baada ya kampeni ngumu iliyowaacha bila taji lolote.
Wanamvinyo hao walio na makazi yao Ruaraka jijini Nairobi, wanatafuta kurejea kwa nguvu katika msimu ujao na tayari wameanza shughuli ya usajili wakisaka wachezaji watakaowawezesha kuwa washindani wakuu katika kampeni ijayo.
Walipata wakati mgumu katika mzunguko wa pili wa msimu, hasa baada ya kuumia kwa Ryan Ogam, ambaye alikuwa amefunga mabao 15 katika mzunguko wa kwanza.
Ogam alikosa karibu mzunguko mzima wa pili baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti na alirejea uwanjani kwa dakika 45 pekee katika mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Kakamega Homeboyz.
Okere amesema wanatilia mkazo safu ya ushambuliaji wanapojenga kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao.
“Wakati Ryan (Ogam) alipoondolewa kwa majeraha, tuliteseka kupata mabao msimu huu uliopita. Imetuonyesha kuwa hili ni eneo tunalopaswa kuwekeza. Tayari tumeanza mazungumzo na baadhi ya walengwa tuliowatambua, na tunataka kuwaleta wachezaji wanaoweza kutufungia angalau mabao 10 au zaidi kila msimu,” kocha huyo alisema.
“Kama tungekuwa makini kwenye safu ya ushambuliaji, naamini tungekuwa tukipambana kuwania ubingwa hadi siku ya mwisho na huenda tungeushinda. Safu ya mbele imekuwa sehemu yetu dhaifu zaidi, hasa katika mzunguko wa pili,” Okere aliongeza.
Klabu hiyo imekuwa ikifuatilia chaguzi mbalimbali za washambuliaji, wakiwemo Moses Shummah kutoka Kakamega Homeboyz na Emmanuel Osoro wa FC Talanta.
Hata hivyo, wawili hao wameponyoka mikononi mwao, wakichagua kusaka uhamisho wa muda mrefu kuelekea Zambia.