
Mshambuliaji wa Kenya, Michael Olunga, amejiunga rasmi na klabu ya Al Arabi SC ya Qatar kwa mkataba wa miaka miwili, hatua inayowakilisha sura mpya muhimu katika taaluma yake ya soka iliyopambwa na mafanikio.
Olunga anakuwa Mkenya wa pili kuchezea Al Arabi, akifuata nyayo za Dennis Oliech, ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Uhamisho wa Olunga unafuatia kipindi cha mafanikio cha miaka minne katika klabu ya Al Duhail SC, ambako aliaga akiwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo, akifunga jumla ya mabao 130 katika michuano yote.
Uwezo wake wa kufumania nyavu ulimfanya atambe katika Ligi Kuu ya Qatar (Qatar Stars League), akiisaidia Al Duhail kutwaa mataji kadhaa huku akivutia heshima na pongezi kutoka pande zote.
Kabla ya mafanikio yake nchini Qatar, Olunga alikuwa amewika katika ligi mbalimbali duniani mbali na kipindi chake katika vilabu tofauti vya Ligi Kuu ya Kenya.
Akiwa Japan, alishinda Kiatu cha Dhahabu cha Ligi ya J1 mwaka 2020 baada ya kufunga mabao 28 akiwa na Kashiwa Reysol na pia alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu (MVP).
Msimu wa mwaka 2019 katika Ligi ya J2 ulikuwa wa kusisimua pia, alikifungia klabu hiyo mabao 27.
Katika soka ya kimataifa, aliwahi pia kucheza Uhispania akiwa na Girona, Sweden katika klabu ya Djurgården, na China na klabu ya Guizhou Heng Feng.
Kwa sasa, tetesi kuhusu mustakabali wake zimefikia kikomo, na Olunga anakumbatia changamoto mpya akiwa na Al Arabi, ambao wanatumai mshambuliaji huyo mrefu ataendeleza ubabe wake wa kufunga mabao na kuongoza juhudi za klabu hiyo katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Akiwa na jumla ya mabao 273 katika zaidi ya mechi 320 za klabu alizochezea katika taaluma yake, Olunga bila shaka ni mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kutoka Afrika.
Ustadi wake wa kufunga, uwezo wa kuzoea mazingira mapya, na wepesi wake mbele ya lango vimemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wa kuaminika zaidi katika historia ya soka ya Kenya.
Ingawa Olunga anatarajiwa kukosa mashindano ya CHAN 2024, mashabiki bado wana matumaini kuwa nyota huyo ataendelea kuimarika na kuleta mchango muhimu katika kampeni ya Harambee Stars ya kufuzu Kombe la Dunia la 2026 katika mechi zijazo za kimataifa dhidi ya Gambia.