
Nahodha wa Harambee Stars, Aboud Omar, ameonyesha matumaini makubwa huku kikosi hicho kikijitayarisha kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN), litakalofanyika nchini kwa mara ya kwanza katika historia.
Zikiwa zimesalia siku 20 kabla ya kipenga cha kwanza kupulizwa tarehe 3 Agosti, shauku na matarajio yamezidi kupanda nchini.
Harambee Stars wataanza kampeni yao kwa mchuano wa kusisimua dhidi ya DR Congo katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani.

Katika mahojiano maalum, Omar alisisitiza kuwa jukumu lake kama nahodha lina uzito mkubwa kwani wanawakilisha taifa zima.
"Hatuchezi kwa niaba yetu pekee. Tunabeba matumaini na ndoto za Wakenya wote wanaotaka kuona mafanikio ya timu yao katika kiwango cha bara," alisema Omar.
Nahodha huyo aliahidi kuwa kikosi cha Stars kitajitahidi kufika fainali na kushinda ubingwa, huku akiwaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwapa nguvu.
"Mashabiki wafike kwa wingi na kupaza sauti zao kwa nguvu. Tumejipanga kufika fainali na kuibuka mabingwa," aliongeza.

Omar alisema maandalizi yanaendelea vizuri, na kwamba timu inaendelea kufanyia kazi mikakati ya kiufundi na kimbinu ili kuwa tayari kwa michuano hiyo mikali.
"Hadi sasa maandalizi yanaridhisha. Tunaongeza juhudi kila siku ili tutakapokutana na wapinzani wetu tuwe tayari kabisa," alisema.
Kocha wa Harambee Stars Benni McCarthy Atangaza Kikosi cha Muda kwa CHAN 2024
Alibainisha pia kuwa wachezaji wengi walioko kwenye kikosi wanawakilisha Kenya kwa mara ya kwanza, na wana ari ya juu ya kuonyesha uwezo wao katika jukwaa la kimataifa.
Mashindano ya CHAN yanayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) yatahusisha mataifa 16, lakini macho yote yatakuwa kwa Kenya kama wenyeji wa michuano hiyo.

Rais wa FKF, Hussein Mohamed, aliunga mkono kauli ya Omar, akihimiza mashabiki wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu ya taifa.
"Tujitokeze kwa wingi kwa ajili ya vijana wetu. Tujaze Kasarani, tuwapigie debe na tuwaunge mkono kuanzia dakika ya kwanza," alisema Hussein.
CHAN itafanyika Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu Rwanda ilipokuwa mwenyeji mwaka 2016.
Maafisa wa michezo nchini wanaamini kuwa Kenya ina nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuwa mwenyeji wa mashindano ya hadhi ya juu.
Kadiri siku zinavyosonga, presha na matarajio vinaongezeka. Mchezo wa ufunguzi kati ya Kenya na DR Congo utatoa mwelekeo wa kampeni ya Harambee Stars.
Mashabiki wanahimizwa kununua tiketi mapema na kuugeuza Uwanja wa Kasarani kuwa ngome ya taifa.
"Huu ndio wakati wetu. Dunia inatuangalia — na historia inatungoja," ikasema taarifa ya FKF.