logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ruto Awasihi Wakenya Kudumisha Nidhamu Wakati wa Mechi ya Harambee Stars

Rais atoa wito wa amani na mshikamano kabla ya mtanange wa CHAN 2024.

image
na Tony Mballa

Michezo15 August 2025 - 18:28

Muhtasari


  • Rais William Ruto ametoa onyo kwa mashabiki wa soka nchini kuzingatia nidhamu na kuepuka vurugu wakati Kenya ikijiandaa kuivaa Zambia kwenye michuano ya CHAN 2024, akisisitiza kuwa taswira ya taifa inategemea utulivu wao.
  • Akiwahutubia mashabiki wa Harambee Stars, Rais Ruto amewataka kuonyesha mshikamano na heshima wakati wa mechi dhidi ya Zambia, akionya kuwa vurugu au utovu wa nidhamu utaharibu jina la Kenya katika mashindano ya CHAN 2024.

NAIROBI, KENYA, Agosti 15, 2025 — Rais William Ruto ametoa wito kwa mashabiki wa soka nchini kuhakikisha utulivu na kufuata kikamilifu sheria za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) wakati wa mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN) itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani.

Ruto alionya kwamba vurugu zinaweza kuharibu nafasi ya Kenya kama mwenyeji wa kuaminika wa mashindano makubwa.

Rais William Ruto

Ruto: Tuelimishe Mashabiki na Kulinda Heshima ya Taifa

Ruto alisema, “Mimi nawaomba Wakenya, tafadhali tusichome mechi, tuhakikishe kwamba tunafuata taratibu kuambatana na sheria za CAF.”

Alibainisha kuwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi na Wizara ya Michezo zitaanzisha maeneo maalum ya mashabiki (fan zones) jijini Nairobi na maeneo mengine nchini, yatakayowekwa skrini kubwa za moja kwa moja ili kutoa fursa kwa wale wasio na tiketi kufuatilia mechi kwa usalama.

Alisifu mashabiki kwa kuunga mkono Harambee Stars kwa nguvu na ari, lakini akasisitiza umuhimu wa nidhamu.

“Wale wenye tiketi lazima wawe na mpangilio mzuri, na wale wasio na tiketi bado watafurahia mechi kutoka maeneo yaliyotengwa kwa mashabiki. Tuhifadhi nafasi ya timu yetu na heshima ya nchi yetu,” aliongeza.

CHAN 2024: Hatua ya Kihistoria kwa Kenya

Ruto alisisitiza kuwa Kenya kuandaa CHAN kwa mara ya kwanza ni hatua muhimu kuelekea kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambalo Kenya itashirikiana na mataifa jirani kulihost.

“Tunaongeza juhudi ili Kenya icheze kwenye ligi sahihi ya mataifa makubwa ya michezo,” alisema.

Wito wa Ruto unakuja baada ya kauli kama hizo kutolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano, Nicholas Musonye, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, na wachezaji wa Harambee Stars.

Rais William Ruto

Maeneo Sita Maalum kwa Mashabiki wa Soka

Jumla ya maeneo sita rasmi ya mashabiki yameanzishwa jijini Nairobi ili kupunguza msongamano mkubwa katika Uwanja wa Kasarani. Maeneo hayo ni Uhuru Park (CBD), Lucky Summer–Ngomo (nyuma ya Kasarani Stadium), Uwanja wa Dandora, Utalii (Stima Club), Jacaranda Grounds, na Kibera DC Grounds.

Waziri wa Michezo Salim Mvurya alisema, “Maeneo haya ya mashabiki yataleta hali ya uwanjani karibu na watu, huku yakitusaidia kudhibiti idadi ya mashabiki wanaoingia Kasarani kwa kuzingatia masharti ya CAF.”

Skrini kubwa zitawekwa katika kila eneo, huku usalama ukiimarishwa kwa uwepo wa maafisa wa polisi wa kutosha ili kuhakikisha utulivu na usalama wa mashabiki.

Sababu ya Hatua Hii: Tahadhari Baada ya Vurugu

Uamuzi wa kuanzisha maeneo haya ulifikiwa baada ya mkutano wa usalama wa juu uliohudhuriwa na Mkuu wa Usalama wa CAF, Christian Emeruwa, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, na maafisa wakuu wa usalama.

Hatua hii inalenga kuepusha marudio ya vurugu zilizoshuhudiwa Agosti 10 wakati Kenya ilipokutana na Morocco kwenye mechi ya hatua ya makundi.

Katika mchezo huo ulioishia kwa ushindi wa 1-0 kwa Harambee Stars, vurugu ziliibuka ambapo milango ilivunjwa, mashabiki wasio na tiketi waliingia kwa nguvu, maeneo yaliyopigwa marufuku yalivamiwa, na msongamano mkubwa ulihatarisha maisha.

Nje ya uwanja, ripoti zilionyesha polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kudhibiti umati.

Faini na Onyo Kali Kutoka CAF

Kutokana na matukio hayo, CAF iliipiga Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) faini ya Sh6.45 milioni (Dola 50,000) kwa ukiukaji wa masharti ya usalama na kutoa onyo kuwa tukio kama hilo likijirudia, mechi za timu ya taifa zinaweza kuhamishiwa ugenini au Kenya kunyimwa nafasi ya kuandaa mashindano ya kimataifa.

Aidha, CAF ilitoza faini ya Sh644,500 kwa tukio la msongamano na kuingia bila ruhusa wakati wa mechi dhidi ya DR Congo, na Sh1.29 milioni kwa tukio la kushambulia na kuwazuia maafisa na wageni wa CAF.

Rais William Ruto

Masharti Mapya ya CAF kwa Mechi ya Jumapili

Kwa mujibu wa maagizo mapya ya CAF, idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia Kasarani Jumapili imepunguzwa hadi asilimia 60 ya uwezo wa uwanja, takribani mashabiki 27,000 pekee.

Kuingia uwanjani kumeruhusiwa kwa wenye tiketi za kidijitali pekee, huku tiketi zilizochapishwa kwa njia ya kawaida (thermal-printed) zikibandwa marufuku.

Kamati ya Maandalizi ya Mashindano imeagizwa kuendesha kampeni ya uhamasishaji umma kuhusu kanuni hizi mpya.

Kuelekea Jumapili: Usalama Kwanza

Viongozi wote, wakiwemo Ruto, Musonye na Mvurya, wameweka wazi kuwa lengo kuu ni kulinda usalama wa mashabiki, wachezaji, na heshima ya taifa. Wamesisitiza kuwa kila shabiki ana nafasi ya kufurahia mechi bila kuhitaji kuvunja sheria.

Jumapili, macho ya bara zima yatakuwa Kasarani, si tu kushuhudia kipimo cha soka, bali pia kuona kama Kenya inaweza kusimamia hafla kubwa kwa ustadi, usalama na nidhamu.

Makala Zinazohusiana

Maarufu Zaidi

RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved