Hali ya mshtuko na huzuni ilitanda katika kijiji cha Umiru, katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya baada ya mhitimu mmoja wa shahada ya Sayansi ambaye alimaliza shule takriban miaka mitano iliyopita kupatikana amefariki ndani ya bafu.
Bi Vera Omondi ambaye alihitimu kutoka chuo kikuu cha Masinde Muliro mwaka wa 2019 anaripotiwa kujitoa uhai mnamo Januari 11, 2024 baada ya kukosa kupata kazi licha ya kutuma maombi mengi.
Mwili wa marehemu ulipatikana na mama yake, Herine Okoth, ukining’inia ndani ya bafu nyumbani kwa wazazi wake huku ukiwa amefungwa kamba shingoni. Stakabadhi zake za masomo pia zilipatikana zimewekwa kwenye kitanda chake.
Marehemu hata hivyo hakuacha barua yoyote ya kujitoa uhai.
Bw Cleti Kimaiyo ambaye ni kamanda wa polisi wa Kaunti ya Siaya alithibitisha kisa hicho huku akibainisha kuwa mamake marehemu alikuwa ameenda kumwamsha wakati alipogundua kuwa hakuwa chumbani mwake. Kisha alichukua hatua ya kumtafuta bintiye alipokuta mwili wake uliokuwa ukining'inia bafuni, jambo ambalo lilimshtua sana.
Bosi huyo wa polisi alisema uchunguzi ulibainisha kuwa usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi, marehemu na mama yake walizungumza kuhusu hali yake ya kukosa kazi. Vera alikuwa ametuma maombi ya kazi zaidi ya 500 tangu amalize shule lakini hakuwa amebahatika kupata kazi yoyote.
Mwili wa marehemu baadaye ulihamishwa hadi katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Yala ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti huku uchunguzi kuhusu kifo hicho ukianza.