Multichoice Kenya, kampuni inayoongoza kwa burudani Barani Africa, imezindua kipindi kipya cha televisheni cha Kenya “Shanga” katika hoteli Maasai Lodge, Kaunti ya Nairobi.
Kipindi kipya kitachukua nafasi ya ‘Salem’ na kitaonyeshwa kila Jumatatu hadi Ijumaa kwenye Maisha Magic Plus, inayopatikana kwenye DStv Channel 163 na GOtv Channel 3 saa 8:00 usiku.
Kipindi cha Shanga kinamshirikisha Brahim Ouma aliyetamba katika kipindi cha ‘Pepeta' kinachopeperushwa kupitia tovuti ya burudani ya Showmax na Foi Wambui aliyejizolea umaarufu kupitia kipindi cha ‘Salem’.
Kipindi cha Shanga kinahusu Soilan, binti wa jamii ya Wamaasai. Wakati Naibei anataka kumuoa kwa nguvu, Soilan anaonyesha ujasiri kwa kukataa - hali inayosababisha mshtuko kijijini. Ukaidi huu unasababisha makabiliano katika sherehe ya ‘Eunoto’ - hafla muhimu katika jamii ya Wamaasai ambapo vijana wa kiume hunyolewa nywele ishara ya kuvuka kutoka utoto hadi utu uzima - kati ya Naibei na Moran maarufu anayeitwa Ledama.
Filamu hii inawahusisha wahusika watatu wakuu, katika kufuata ndoto zao, wanajikuta wamenaswa katika hali ngumu ya mapenzi. Matarajio na changamoto zao zinaonyeshwa waziwazi katika simulizi . Utajiri wa utamaduni wa Wamaasai pamoja na 'maudhi' yake vimejitokeza wazi katika filamu hii.
Mkurugenzi Mkuu wa MultiChoice Kenya, Nzola Miranda, alisema kuwa kampuni hiyo itazidi kufadhili filamu zinazotengenezwa humu nchini na zinazoangazia jamii zetu.
"Leo ni hatua ya kusisimua kwa watazamaji wetu tunapotambulisha rasmi filamu ya 'Shanga'.. Tumejitolea kikamilifu kukuza talanta na filamu zinazotengenezwa humu nchini ili kuhifadhi utamaduni, na pia kuunda nafasi za ajira kwa Wakenya,” akasema Bw Miranda
"Multichoice Kenya tukiwa vinara wa filamu zinazopendwa zaidi nchini Kenya, tunajivunia kuwa na maktaba kubwa zaidi ya vipindi na filamu zilizotengenezwa humu nchini na Wakenya. Filamu za humu nchini zinakuza utamaduni wetu na kuwapa nafasi za ajira maelfu ya Wakenya.”
Kipindi cha Shanga kinaingia kwenye orodha ya vipindi vilivyozinduliwa na MultiChoice Kenya tangu Januari mwaka huu.
Vipindi vingine ni kama vile 'Kam U Stay', kilichotambuliwa kama Kipindi Bora cha Ucheshi katika Televisheni katika katika Tuzo za Kalasha, na'Haki Mwitu.'
“ Dhamira yetu ni kuendelea kutayarisha na kupeperusha vipindi vya humu nchini na kuunga mkono Tume ya Filamu ya Kenya na Serikali kukuza filamu vya hapa nchini. Tutaendelea kushirikiana na makampuni ya kutengeneza filamu ili kuunda vipindi bora ambavyo vitakuwa na mvuto na kuvuma katika rubaa za kimataifa. Kupitia ushirikiano wa tasnia nzima, watengenezaji wetu wa filamu watatambuliwa katika majukwaa ya kimataifa," aliongeza Bw. Miranda.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano Mwema wa MultiChoice Kenya, Elisha Kamau, alisema filamu ya Shanga iliashiria kujitolea kwa kampuni hiyo kuendelea kuwekeza katika sanaa na kukuza vipaji nchini Kenya.