Beki matata wa Uhispania, Sergio Ramos, amejiunga rasmi na klabu ya Monterrey ya Mexico na kuchagua kuvaa jezi namba 93, uamuzi unaobeba maana kubwa katika historia yake ya soka.
Chaguo lake la namba ya jezi sio la bahati mbaya bali linahusiana moja kwa moja na moja ya nyakati muhimu zaidi katika taaluma yake, haswa wakati alipokuwa mchezaji wa Real Madrid.
Ramos amehusisha namba 93 na goli lake maarufu alilofunga katika dakika ya 93 kwenye fainali ya UEFA Champions League mnamo Mei 24, 2014.
Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Lisbon, Ureno, Real Madrid ilikuwa nyuma kwa goli 1-0 dhidi ya Atlético Madrid hadi Ramos alipoisawazishia timu yake kwa kichwa murwa baada ya krosi ya Luka Modrić.
Bao hilo lilisababisha mechi kuingia muda wa nyongeza, ambapo hatimaye Real Madrid iliibuka na ushindi wa 4-1, ikinyakua taji lao la 10 la UEFA Champions League, maarufu kama La Décima.
Ushindi huo ulikuwa wa kihistoria kwa klabu hiyo, na bao la Ramos lilikuwa miongoni mwa matukio yasiyoweza kusahaulika katika historia ya soka.
Katika mahojiano yake baada ya kusajiliwa na Monterrey, Ramos alieleza kuwa jezi namba 93 ni ishara ya mafanikio na mapambano aliyopitia akiwa mchezaji wa Real Madrid. Hili linadhihirisha jinsi alivyopania kuhifadhi kumbukumbu hiyo hata anapoanza safari mpya nchini Mexico.
"Dakika ya 93 ina maana kubwa kwangu. Ilikuwa wakati wa ushindi wa kihistoria na sehemu ya urithi wangu kama mchezaji. Nataka kuiheshimu na kuiendeleza popote ninapocheza," alisema Ramos.
Baada ya Ramos kutangaza kuchagua namba 93, klabu yake ya zamani Real Madrid ilitoa ujumbe wa pongezi na kuonyesha fahari kwa mchezaji wao wa zamani.
Kupitia mitandao ya kijamii, Madrid ilituma ujumbe ukisema, "Dakika yetu ya 93 itabaki kuwa ya kipekee milele. Kila la heri, Sergio Ramos."
Hii ilionyesha jinsi bao hilo bado linavyothaminiwa na klabu pamoja na mashabiki wa Real Madrid.
Hatua ya Sergio Ramos kuchagua jezi namba 93 katika klabu yake mpya ya Monterrey si ya kawaida.
Ni uamuzi unaoonyesha heshima kwa historia yake, ushindi wake mkubwa na ari yake ya kupambana uwanjani.
Mashabiki wa soka kote ulimwenguni wanatarajia kuona kama
atafanikiwa kuendeleza urithi huo katika Ligi ya Mexico.