
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema ana matumaini Kai Havertz atarejea uwanjani mapema kuliko ilivyotarajiwa, kufuatia maendeleo mazuri ya nyota huyo wa Ujerumani anayepambana kupona jeraha la msuli wa paja.
Havertz alitarajiwa kukosa msimu mzima baada ya kufanyiwa upasuaji mwezi Februari, alipoumia wakati wa kambi ya mazoezi ya hali ya joto mjini Dubai.
Ingawa hawezi kurejea kwa muda wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Paris Saint-Germain, Arteta anaamini kiungo huyo anaweza kuwa tayari iwapo Arsenal watafuzu hadi fainali itakayopigwa mjini Munich, Mei 31.
“Kwa nusu fainali? Nafikiri hiyo ni mapema sana,” Arteta alisema. “Lakini kama ningelazimika kubashiri iwapo atarudi mapema kuliko ilivyotarajiwa, ningesema: ‘Ndiyo’.
“Anavyofanya kazi kila siku—yupo ukumbini akijifua, anawasukuma wote—sioni kama kuna kitu kinachoweza kumzuia tena.”
Arsenal walifanikiwa kufuzu kwa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009, baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Real Madrid, licha ya kutowajumuisha Havertz na Gabriel Jesus.
Ufanisi huo wa Ulaya umewafariji mashabiki huku matumaini yao ya ubingwa wa Ligi Kuu ya England yakizidi kufifia. Arsenal wako njiani kumaliza nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo, wakiachwa pointi 13 nyuma ya vinara Liverpool huku zikiwa zimesalia mechi sita.
Liverpool wanaweza kutawazwa mabingwa mapema siku ya Jumapili iwapo watawashinda Leicester na Arsenal wapoteze dhidi ya Ipswich, walioko chini ya msimamo.
Arteta amewataka wachezaji wake wasilegeze kamba, akisema kuwa nafasi ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao bado haijathibitishwa.
“Tutasimama imara kuhakikisha tunashinda mechi na hilo halitokei,” alisema Mhispania huyo kuhusu uwezekano wa Liverpool kutwaa taji Jumapili. “Tunapaswa kuamka na kuanza kushinda mechi.”