
Wakili wa Kibrazili Larissa Ferrari amemshutumu kiungo wa zamani wa West Ham na timu ya taifa ya Ufaransa, Dimitri Payet, kwa unyanyasaji wa kimwili, kiakili, kisaikolojia na kingono katika uhusiano wa miezi saba ambao ameelezea kuwa wa kiwewe.
Larissa, mwenye umri wa miaka 28 na ambaye ni mama wa watoto wawili, anadai kuwa mchezaji huyo ambaye sasa anachezea Vasco da Gama jijini Rio de Janeiro, alimnyanyasa na kumdhalilisha kwa njia nyingi kwa kipindi chote walichokuwa pamoja.
"Alinifanya niamini kuwa ili tusitengane, lazima nimpende kwa njia yake—hata kama ilimaanisha kujidhalilisha,” Larissa alisema kwa uchungu.
Larissa anasema Payet alianza kumtongoza kupitia akaunti ya bandia ya Instagram. Walikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza katika hoteli moja jijini Rio, ambapo mwanzo ulionekana kuwa wa kimapenzi. Lakini kufikia mwezi Oktoba, Payet alianza kumtaka afanye vitendo vya kudhalilisha, ikiwa ni pamoja na harusi ya bandia na kutuma video za aibu kama uthibitisho wa mapenzi yake.
Larissa anasema alikumbwa na vipigo mara kadhaa, mojawapo akiwa Januari baada ya Payet kurejea kutoka Ufaransa. Alitoa picha za majeraha yake kwa polisi na kusema alikata uhusiano baada ya kupatwa na mshtuko wa hofu mwezi Februari.
Licha ya unyanyasaji huo, alikiri kuwa aliendelea kumuona Payet akiamini kuwa mabadiliko ya tabia yalitokana na mapenzi. Hata hivyo, baada ya kuanza kupata usaidizi wa kisaikolojia, aligundua alikuwa ametumiwa vibaya.
Uhusiano wao uliibuka hadharani mwezi Machi na wiki moja baadaye, Larissa aliwasilisha ripoti rasmi kwa polisi. Tangu wakati huo, amefungua kesi kadhaa na kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kisaikolojia.
Polisi wa Rio de Janeiro wamethibitisha kuwa uchunguzi dhidi ya Payet unaendelea. Larissa pia ameomba hatua za ulinzi zichukuliwe kwa usalama wake.
"Nataka wanawake wengine waweze kutambua dalili za unyanyasaji wa kihisia—hasa wanapokuwa katika mahusiano na wanaume matajiri wenye mvuto wa nje,” alisema.
Payet, ambaye ameoa na ana watoto wanne, bado hajajibu hadharani kuhusu tuhuma hizo.