Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi alikutana na kufanya mazungumzo na Seneta wa Marekani Chris Coons ambaye alimtembelea katika Ikulu ya Nairobi.
Seneta Coons, ambaye anaongoza ujumbe wa bunge la Seneti na Wawakilishi wa Bunge la Marekani, alimpongeza Rais Kenyatta kwa kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo wakati wa uchaguzi.
“Tunatiwa moyo na amani ambayo Kenya imeendelea kuwa nayo katika kipindi hiki,’’ alisema Seneta Coons.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta alisema Kenya itasalia imara katika kusisitizia kanuni za utawala bora ili kuhakikisha nchi inashikilia msimamo wake wa mfano bora wa demokrasia barani kwa kudumisha amani katika kipindi hiki cha mpito’’.
Hamu yangu kuu ni kwamba amani itakuwepo na kuweza kuwa mfano katika bara na ulimwengu,” Rais Kenyatta alisema.
Pia waliokuwepo wakati wa mazungumzo hayo ni pamoja na Waziri mambo ya nje Raychelle Omamo, Waziri wa biashara Betty Maina na Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman miongoni mwa wengine.
Awali, Seneta Coons alifanya mazungumzo na rais mteule William Ruto kuzungumzia uhusiano kati ya Marekani na Kenya.
Mwingine aliyekutana naye ni kinara na Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga kujadili ‘’maadili ya kidemokrasia yanayoshirikishana Kenya na Marekani, kulingana na akaunti ya Twitter ya ubalozi wa Marekani.