Esther Mboone ,25, kutoka Kitale alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mume wake Augustine Baraza ,28, ambaye akitengana naye mwaka jana.
Esther alisema kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika Novemba mwaka jana kufuatia mizozo ya kinyumbani.
"Tulikosana kwa nyumba. Alikuwa haniongeleshi. Kuna mama alikuwa amemkodishia nyumba, alikuwa anatoka kazi anaenda anakaa huko tu anarudi saa mbili usiku. Wakati mwingine alikuwa anarudi saa sita," Esther alisema.
Aliongeza, "Alikuwa anagombana tu. Sasa yeye hanitafuti. Ningependa awaeleze kama ako na haja na mimi ama bado. Nilitoka kwa ndoa mwezi wa kumi na moja nikaenda nyumbani kwetu. Nilimpenda tu sana. Mimi nampenda sana lakini yeye sioni kama ananipenda."
Esther alikiri kwamba anampenda sana Baraza ila ana wasiwasi mkubwa kuwa yeye hampendi.
Aidha, alidokeza kuwa wakwe zake waliipinga sana ndoa yao, jambo jingine lililochangia yeye kutoroka.
"Nilikaa naye miezi tisa hivi. Alikuwa wa maana kwa maisha yangu. Watu wa kwao waliingilia hii ndoa sana," alisema.
Kwa bahati mbaya, Patanisho iligonga mwamba kwani Bw Baraza hakupatikana kwa simu.
Kufuatia hayo, Esther alisema, "Sasa mimi nishamove on basi. Kweli ni kama watu wao hawanitaki. Nilipotoroka ata sikumwabia, nilifunganya virago vyangu na nikatoka."
Aidha, alisema kuwa ana hakika kuwa mume huyo wake wa zamani bado hajapata mwanamke mwingine.
"Tulienda tukatembea kwao na dada yangu tukapata bado hajapata mtu mwingine," Alisema.
Alipopewa nafasi ya kuzungumza na Baraza hewani, Esther alisema, "Nilikupenda tu sana. Roho yangu ilikuwa imeishia kwako. Lakini wewe sioni kama unanipenda."