Mwanamke aliyejitambulisha kama Rosemary Mukami Njeru (35) kutoka kaunti ya Embu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Peter Ng'ang'a (50) ambaye ametofautiana naye.
Rosemary alisema alianza kukosana na mume wake Agosti mwaka huu baada ya kutofautiana kuhusu suala la kazi.
Alisema mumewe amekuwa hataki aende kazi ilhali anahitaji pesa za kumsaidia mtoto wake wa kwanza ambaye aliacha nyumbani.
"Mume wangu Hataki nikienda kushuka wateja kwao. Huwa naenda kushuka watu juu sijaweka saluni yangu. Nilijaribu kumueleza akasema wateja wakuje nyumbani badala ya mimi kuenda. Hataki nitoke," Rosemary alisema.
Aliongeza, "Kuna siku nilienda kufanya mtu blowdry, nikapata amefunga nyumba na ameenda na funguo. Alisema wakati mwingine nikienda nitapata ametupa manguo zangu nje. Tuko tu kwa nyumba lakini kazi ndio shida."
Juhudi za kumpatanisha Rosemary na mumewe kwa bahati mbaya hazikufaulu kwani Bw Ng'ang'a hakushika simu yake.
Rosemary aliendelea kusisitiza kuhusu umuhimu wa yeye kuenda kazini huku akidai kwamba yeye ndiye anasimamia mahitaji yote ya mtoto wake wa kwanza.
"Sitaki kukaa nyumbani, nataka kufanya kazi. Mtoto mwenye ako nyumbani ni mimi namlipia shule," alisema.
Je, maoni ama ushauri wako kuhusu Patanisho yako ni upi?