Wiki hii kampuni ya michezo ya ubashiri na bahati nasibu Sportpesa ilitangaza mshindi mpya wa Jackpot ya katikati ya wiki.
Kupitia kurasa za mitandao yao ya kijamii, Sportpesa walimtangaza mwanaume mmoja kwa jina John Muiru kuwa mwenye bahati ya nyota ya katikati mwa wiki kwa kujinyakulia kitita cha milioni 38 na ushee.
Muiru ambaye alikuwa amependekezwa kama mmoja wa mawaziri wa kaunti ya Nyandarua katika kitengo cha ardhi, mipango na ukuzaji wa miji alitangazwa mshindi na kufika katika makao makuu ya kampuni hiyo li kukabidhiwa kitita chake.
Muiru alitambulishwa kama mtu wa tano kushinda Jackpot baada ya kushinda Ksh 38,792,902 mnamo Alhamisi, Oktoba 27, 2022.
Alijiwasilisha katika afisi za Sportpesa mnamo Jumamosi, Oktoba 29, 2022, siku moja baada ya kuhudhuria mchujo wa saa moja katika Bunge la Kaunti ya Nyandarua.
Akizungumza katika afisi za Sportpesa, Muiru alikiri kuwa Mungu ndiye kitovu cha mafanikio yake kufuatia habari njema alizopokea.
"Yote ni Mungu kwa sababu sijawai kuajiriwa tangu kuachishwa kazi wakati wa mripuko wa Covid-19. Maisha yamekuwa magumu tangu wakati huo lakini leo nina furaha sana. Katika wiki mbili zilizopita mambo mazuri yamekuwa yakitokea katika maisha yangu na ndivyo ilivyo. kama ndoto," Muiru alisema huku tabasamu zikimponyoka usoni.
Alipoulizwa jinsi anavyopanga kutumia pesa hizo, Muiru ambaye alibainisha kuwa kwa sasa anakodolea macho jackpot ya SportPesa Mega ambayo kwa sasa ni Ksh258,230,739 alisema kwamba anakusudia kurudisha pesa kwa shughuli nzuri kwa kusaidia mwanafunzi wa seminari kwa masomo.
