
MWINJILISTI Ringtone Apoko amejitolea kumpa hifadhi nyanyake aliyekuwa TikToker, Brian Chira katika jumba lake la kifahari la mtaani Runda baada ya bibi huyo kusema kwamba anakoishi hakuna usalama wa kutosha.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ringtone alichapisha video
akiwa mbele ya jumba lake barazani na kusema kwamba yuko tayari kuishi na bibi
huyo huko Runda ambako kuna usalama wa kutosha.
Aidha, Ringtone alimtahadharisha bibi huyo kuwa makini na
vijana wa TikTok akidai kwamba wanamchezea na asingependa kuona wakiendelea
kumfanyia shere.
“Shosho wa Chira, hawa
vijana wa TikTok wanakuchezea sana, mimi nakupenda. Sasa fanya hivi, kama
mahali ile nyumba ulijengea na unaona hauna raha kule, nakukaribisha uje uishi
na mimi hapa Runda. Nitakupatia ‘main house’ na mimi nitahamia ‘servant quarter’,” Ringtone alisema.
Tamko la msanii huyo aliyepata umaarufu zaidi ya miaka 15
iliyopita kupitia kibao cha ‘Pamela’ linakuja kipindi ambapo nyanyake Chira
amekuwa katika majibizano makali ya tiktokers baada ya kudai kwamba anawazia
kuuza nyumba waliyomjengea.
Tiktokers walikusanya zaidi ya milioni 8 pesa za Kenya mwezi
Machi mwaka jana na kutumia sehemu yazo kumjengea bibi huyo nyumba kumuenzi
Chira ambayo waliipa jina Chira Clan.
Hata hivyo, wiki mbili zilizopita, bibi huyo alijitokeza
akisema kwamba eneo iliko hiyo nyumba si eneo salama na kusema kwamba anawazia
kuiuza ili kuhamia sehemu salama zaidi.
Bibi huyo alisema kwamba kama TikTokers hawatomruhusu kuiuza
nyumba, basi wanafaa kuketi chini kwa mara nyingine tena ili wamfikirie na
usalama wake, akipendekeza kwamba itakuwa bora zaidi kama watamzungushia ua la
umeme kwenye nyumba hiyo.
Tangu kipindi hicho cha moja kwa moja, bibi huyo amekuwa mada
motomoto kwenye TikTok, huku wengi wakihoji kwa nini alionekana kukosa
shukrani, huku wengine wakipendekeza kuwa kulikuwa na masuluhisho bora ya
ukosefu wa usalama kuliko kudai nyumba mpya kabisa.
Mmoja wa wale waliomkosoa waziwazi ni msaidizi wake wa
zamani, Baba Talisha, ambaye alimsuta kwa kile alichotaja kuwa kutokuwa na
shukrani moja kwa moja kwa jamii ya TikTok ambayo ilikuwa imempitia.