
GAVANA wa zamani wa Meru, Kawira Mwangaza na mumewe Murega Baichu wamejirudi katika ufugaji wa nyuki na uvunaji wa asali, siku mbili tu baada ya ugavana kumtoka Mwangaza rasmi.
Wawili hao walionekana kwenye shamba lao la nyuki wakitalii
mizinga na Mwangaza kuthibitisha kwa Maelezo ya picha kwamba walikuwa katika
harakati ya kuvuna asali.
“Jumatano ya kuvuna
asali,” Mwangaza alisema.
Gavana huyo wa zamani alifuatisha maandishi hayo na kifungu
cha Biblia akionekana kujitoa Imani kwamba licha ya masaibu mengi ambayo
yamesababisha kubanduliwa kwake kama gavana, bado ana Imani ya kuiona kesho
njema.
“Wafilipi 4:7, “Na amani
ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo
Yesu.” Askofu Mwangaza aliongeza.
Kuonekana kwake shambani na mumewe kunajiri chini ya saa 24
baada ya kutoa taarifa kuzungumzia anachokihisi kilichangia kubanduliwa kwake
ofisini kama bosi wa kaunti.
Kwa mujibu wake, anahisi kabisa jamii ya Meru imetawalwa na
taasubi ya kiume akidai kwamba wanaume wengi vigogo wa kisiasa katika kaunti
hiyo walipatwa na mchecheto kuona mama akiwa gavana.
“Ajenda kuu haikuwa
kuhusu maendeleo na miradi ya Meru bali ilikuwa ni kuniondoa afisini kwa sababu
wapinzani wangu walihisi nitawabwaga katika uchaguzi ujao wa 2027 kutokana na
historia yangu ya maendeleo katika Kaunti hii ya Meru nimechapa kazi bila
uwoga’’ Mwangaza alisema.
Mwangaza kabla awe Gavana
alikuwa mwakilishi wa kike wa Meru ambapo alianza kupalilia uongozi wake
ifaavyo na akauchukua Ugavana wa Meru kama muaniaji Huru akiwabwaga washindani
wake wa karibu Kama Kiraitu Murungi na Mithiika Linturi.
Hata hivyo, nyota yake ya kisiasa imo katika hatari ya
kufifishwa kabisa baada ya mahakama ya juu kuidhimisha uamuzi wa seneti
kumbandua ofisini, tumaini pekee likisalia kuwa rufaa yake mahakamani dhidi ya
uamuzi huo.
Tayari, Meru imepata gavana mpya – Isaac Mutuma ambaye
aliwania na Mwangaza kama naibu wake katika uchaguzi wa 2022 waliposimama kwa
tikiti ya chama huru.