
TIKTOKER Baba Talisha amekuwa mtu wa hivi punde kuzungumzia kuhusu uozo unaoendeshwa na uraibu wa Kamari katika jamii haswa katika mitaa ya maisha ya chini mijini.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Baba Talisha amewashauri
vijana – ambao kiuhalisia ndio nguvu kazi ya taifa, kukoma kuwa na fikira
kwamba Kamari inaweza kuwa njia ya kujitajirisha.
Mpiga picha huyo alishauri kwamba Kamari hakuna siku
itakufanya kuwa tajiri na badala yake itafyonza kile kidogo ulicho nacho, na
kuwaasa vijana kufuta program zote za kucheza Kamari kwenye simu zao.
Alitilia mkazo akisema kwamba program za Aviator ndizo ambazo
zimeleta madhara makubwa ya kisaikolojia kwa vijana na kuwataka kutumia muda
wao vizuri katika kujituma kutafuta riziki kwa njia halali nay a haki badala ya
kutegemea Kamari.
“Hakuna njia ya mkato
katika maisha, futa hizo program zote za Kamari kwenye simu yangu kijana kisha
ujitume. Kwanza hiyo ya Aviator,” Baba Talisha alisema.
Ushauri wa Baba Talisha unajiri wiki moja baada ya bunge la
kaunti ya Nairobi kuanzisha mchakato wa kujadili mswada unaolenga kudhibiti
masuala ya Kamari haswa kwenye mitaa duni.
Mswada huo unaofadhiliwa na MCA wa Ngara Chege Mwaura
unalenga kuweka masharti makali kwa waendeshaji wa maduka ya Kamari mitaani,
ambapo ikiwa sheria zitakiukwa, waendeshaji wa maduka ya Kamari wanaweza pigwa
faini ya hadi milioni moja au miaka 5 jela.
Madhumuni ya mswada huo kulingana na Chege ni kusaidia
kudhibiti shughuli za kamari na michezo ya kubahatisha katika maeneo yasiyo
rasmi kando na kusaidia kaunti kubuni nafasi za kazi na kuongeza makusanyo ya
mapato.
Waendeshaji wa mashine za michezo ya kubahatisha na wamiliki
wa majengo wanamofanyia kazi ndio waathirika wakubwa kwani kaunti inalenga
kufanya shughuli hiyo kuwa mradi wa gharama kubwa.
Sheria inayopendekezwa inalenga kuanzisha Bodi ya Kaunti ya
Jiji la Nairobi ya Kudhibiti Kamari, Bahati Nasibu na Michezo, ambayo itakuwa
na jukumu la kutoa leseni kwa shughuli zote za kamari, michezo ya kubahatisha na
bahati nasibu katika kaunti.
Mnamo 2021, marekebisho sawa ya sheria ambayo yalitaka kuzuia
kucheza kamari kwa hoteli za nyota tano yalifutwa na mahakama.