
Alisisitiza kuwa serikali ina wajibu wa kuwalinda wale wanaowalinda Wakenya.
Akizungumza Jumamosi katika Ikulu ya Nairobi alipokuwa mwenyeji wa maafisa wa usalama na wale wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa kutoka kote nchini, Rais aliwahakikishia maafisa hao kuwa watapata ulinzi kamili wanapotekeleza majukumu yao.
“Kila afisa wa polisi anayehatarisha maisha yake kuwalinda watoto wetu, familia zetu, na taifa letu lazima ajue kuwa usalama wake umehakikishwa,” Ruto alisema.
“Wanapolitumikia taifa, serikali ya Kenya chini ya uongozi wangu itahakikisha familia zao na maisha yao pia yanalindwa.”
Alilaani ujasiri unaokua wa wahalifu waliowashambulia polisi siku za hivi karibuni, akionya kuwa vitendo hivyo havikubaliki na havitavumiliwa tena.
“Hatuwezi kuwa na nchi ambapo wahalifu wanawafukuza maafisa wa polisi. Kama maisha ya polisi yako hatarini, basi hakuna mtu aliye salama,” alitangaza.
Ruto alihakikishia kuwa maafisa hao watapewa vifaa vyote vinavyohitajika ili kutekeleza majukumu yao bila woga.
“Huwezi kuwalinda wengine ikiwa wewe mwenyewe huna usalama. Wanaume na wanawake wetu waliovaa sare lazima walindwe na wapewe uwezo wa kuwalinda wengine.”
maafisa wa usalama na wale wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa kutoka kote nchini
Aidha, alitoa agizo kwa maafisa wa usalama kusimamia juhudi za amani na mshikamano katika maeneo yao, akisema wana jukumu si tu la kutekeleza sheria bali pia kuongoza juhudi za mshikamano wa kitaifa.
Kauli za Ruto zinakuja kufuatia matukio ya maafisa kushambuliwa na wahuni wakiwa kazini, ya hivi punde zaidi ikiwa ni wakati wa maandamano ya Jumatano.
Maafisa kadhaa walishambuliwa jijini Nairobi.
Waliohudhuria kikao hicho walikuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Katibu wa Wizara Raymond Omollo, Mkurugenzi Mkuu wa DCI Mohamed Amin, na Naibu Makamishna Wakuu Gilbert Masengeli (APS) na Patrick Tito (KPS).