logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ruto Ataka Wakenya Wamweleze Wanapotaka Aende

Aidha, amewataka Wakenya waache kusisitiza kuhusu kuondoka kwake madarakani.

image
na Tony Mballa

Habari27 June 2025 - 15:52

Muhtasari


  • Ruto alipuuzilia mbali wito unaozidi kuongezeka kutoka kwa viongozi wa upinzani wakimtaka ajiuzulu, akiwataka badala yake watoe mpango mbadala wa maana badala ya kuchochea vurugu na machafuko nchini.
  • Kiongozi huyo wa nchi alitaja kauli za “Ruto lazima aende” kuwa ni maneno matupu yasiyo na maana iwapo hayataambatana na mkakati wa kisheria na wa kujenga.

Rais William Ruto amewataka wapinzani wake kuja na mikakati madhubuti ya kuisaidia nchi kusonga mbele, badala ya kushiriki katika mchezo wa kumlaumu kila mara.

Aidha, amewataka Wakenya waache kusisitiza kuhusu kuondoka kwake madarakani.

Ruto alipuuzilia mbali wito unaozidi kuongezeka kutoka kwa viongozi wa upinzani wakimtaka ajiuzulu, akiwataka badala yake watoe mpango mbadala wa maana badala ya kuchochea vurugu na machafuko nchini.

Kiongozi huyo wa nchi alitaja kauli za “Ruto lazima aende” kuwa ni maneno matupu yasiyo na maana iwapo hayataambatana na mkakati wa kisheria na wa kujenga.

“Kama ni suala la mihula, Katiba tayari imeshatatua na kuweka bayana suala hilo. Unaweza kuwa na muhula mmoja au miwili tu… huwezi kuwa na zaidi ya hapo. Kwa hivyo ni nini hiki kuhusu mihula?” aliuliza Rais.

“Kama ni Ruto lazima aende, basi niambieni mnataka niondoke vipi. Mnamaanisha nini kwa kusema Ruto lazima aende? Niondokeje? Kwa sababu tuna Katiba inayotuongoza,” alisema.

Rais alitoa kauli hizo siku ya Ijumaa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs), kufuatia maandamano yenye vurugu yaliyoibuka katika kaunti kadhaa Jumatano, Juni 25, yaliyosababisha uharibifu wa mali, kupotea kwa ajira, na kujeruhiwa kwa watu kadhaa.

“Kama kweli mnataka Ruto aondoke, tafuteni mpango bora. Vurugu na machafuko hayawezi kuokoa nchi yetu. Tuambiane ukweli,” alisema.

Ruto aliwataka viongozi wa upinzani na wakosoaji wake kuwasilisha sera mbadala zinazoweza kuzidi ajenda ya maendeleo ya serikali yake, ambayo alisema tayari inashughulikia masuala ya ajira na gharama ya maisha.

“Fanyeni jambo la heshima. Tengenezeni mpango bora zaidi ya wangu—mpango unaoleta ajira nyingi zaidi, unaopunguza gharama ya maisha, unaotoa fursa nyingi zaidi kwa vijana wa Kenya,” alisema. “Huwezi kubadilisha mpango unaofanya kazi, unaouchukia, bila kuwa na mpango mwingine.”

Akiwa amejawa na hisia kutokana na kile alichokitaja kuwa uchochezi wa chuki na vurugu, Rais alisisitiza kuwa mabadiliko ya kisiasa lazima yatokane na ushawishi, si uharibifu.

“Naomba tafadhali! Wapumbavu waliobaki Kenya ni wachache sana. Tushawishiane. Mkinishawishi, naweza pia kuacha hii kazi niende nikalime na kusaidia katika usalama wa chakula. Lakini msichome nchi – tafadhali, hatuna nchi nyingine.”

Ruto pia aliwakosoa vikali viongozi wa dini na siasa aliowatuhumu kuchochea machafuko.

“Ningependa kuwauliza viongozi wa dini na wanasiasa wanaohamasisha harakati hizi zinazoelekea kwenye vurugu na machafuko... mpango wenu ni upi?”

Alionya kuwa Kenya iko katika hatari ya kuyumbishwa na machafuko endapo maandamano yataendelea kwa mtindo wa sasa, akisisitiza kuwa nchi ni ya Wakenya wote – si ya Rais pekee au wapinzani wake.

“Tukichukua njia hii, hatutakuwa na nchi. Na nchi hii si ya William Ruto – ni ya sisi sote. Na ikiwa hakutakuwa na nchi kwa William Ruto, basi hakutakuwa na nchi kwa yeyote kati yenu,” alisema.

Kauli za Rais zinajiri kufuatia maandamano ya Juni 25 yaliyosababisha uharibifu mkubwa jijini Nairobi na miji mingine mikuu. Ruto alilaani vurugu hizo, akisema zilifanya maelfu kupoteza riziki zao.

“Tarehe 24 Juni, tulikuwa na watu wengi walio na kazi. Tarehe 25, kazi zao ziliteketea. Halafu kuna watu wanaotuambia tarehe 25 ilikuwa mafanikio. Kweli? Watu wengi wamejeruhiwa, biashara nyingi zimeharibiwa… hiyo ndiyo mafanikio kweli?” alihoji Ruto.

Kutokana na hayo, aliagiza vyombo vya usalama kuharakisha mchakato wa kuwatambua na kuwachukulia hatua wahusika wa machafuko na vurugu za Juni 25, akisisitiza kuwa serikali imejitolea kulinda maisha na riziki za wananchi kwa kufuata sheria.

“Natarajia Inspekta Jenerali wa Polisi na mashirika yote husika ya polisi kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na kwa ufanisi; wahusika wa vurugu na uporaji huu lazima watambuliwe na kushtakiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria, haraka na kwa ukali,” alisema.

Akiomboleza vifo na upotevu wa maisha na mali wakati wa maandamano, Ruto alisema Kenya itasalia kuwa nchi inayotawaliwa na sheria, na matendo ya kihalifu hayatavumiliwa chini ya uongozi wake.

“Kenya ni nchi inayotawaliwa kwa misingi ya sheria, na serikali haitakubali vitendo kama hivyo kuharibu maisha na riziki za wananchi,” aliongeza.

Kauli za Rais zinakuja siku moja baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Alhamisi, Juni 26, 2025, kufichua kuwa wahuni walilenga vituo vya polisi wakati wa maandamano ya kuwakumbuka waathiriwa wa maandamano ya kupinga serikali ya Juni 2024 yaliyosababisha vifo vya watu 60.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved