logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Akothee afunguka masomo mazito kutoka kwa ndoa fupi na Omosh, mvutano wa kifamilia

Akothee ameeleza kuwa alitamani sana kupendwa na kukubaliwa kama binadamu wa kawaida, lakini aliumia.

image
na Samuel Mainajournalist

Mastaa wako20 April 2025 - 09:15

Muhtasari


  • Akothee amefunguka kuhusu matatizo ya afya aliyopitia kutokana na mzigo wa kihisia alioubeba kwa miaka mingi.
  • Katika hali ya kutafuta amani,  alisema alijikuta akivunjika moyo mara kadhaa, ikiwemo baada ya kuachana na Nelly Oaks.

Akothee

Mwanamuziki maarufu Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu matatizo ya afya aliyopitia kutokana na mzigo wa kihisia alioubeba kwa miaka mingi, akisema alijaribu kurekebisha kila mtu katika familia yake na wale waliomzunguka huku akijisahau mwenyewe.

Kupitia ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa Instagram asubuhi ya Jumapili, Akothee alieleza jinsi alivyojaribu kutafuta mapenzi, kukubalika na heshima kutoka kwa jamaa na marafiki, lakini akajikuta akikabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo uliosababisha kuingia hospitalini mara kwa mara.

"Niligundua kilichokuwa kinanipeleka hospitalini mara kwa mara. Nilijaribu kubeba kila mtu mgongoni na nikajisahau kabisa. Nilidhani naweza kurekebisha familia yangu na kila mtu aliyenizunguka," alisema.

Mwimbaji huyo aliendelea kueleza kuwa alitamani sana kupendwa na kukubaliwa kama binadamu wa kawaida, lakini aliumia alipotambua kuwa kwa baadhi ya watu, alikuwa tu chanzo cha pesa na daraja la wao kufikia malengo yao.

Pia aligusia kuhusu uhusiano wake wa awali na mpenzi wake wa muda mrefu Nelly Oaks, akisema kila walipokuwa wakigombana, alihisi huenda uhusiano huo ndio chanzo cha maumivu yake—lakini baadaye akatambua alikuwa hajawahi kuchukua muda kuelewa kiini halisi cha mateso yake.

Katika hali ya kutafuta amani,  alisema alijikuta akivunjika moyo mara kadhaa, ikiwemo baada ya kuachana na mpenzi wake wa muda mrefu Nelly Oaks, kisha baadaye kuingia katika ndoa iliyodumu kwa muda mfupi na Denis Schweizer maarufu kama Omosh — mwanaume ambaye alimweleza kama “narcissist”.

Wawili hao walifunga ndoa Aprili mwaka jana na kutengana kufikia Juni mwaka huo. Anasema uhusiano huo ulimfundisha kuhusu dhuluma za kihisia kama vile udanganyifu na kuchezewa akili (gaslighting).

“Kuvunjika kwa uhusiano na Nelly na kuingia mikononi mwa narcissist ilikuwa somo chungu lakini lenye manufaa. Nilijifunza kuhusu ‘gaslighting’, udanganyifu wa kihisia na mateso ya kiakili. Namshukuru sana, ilikuwa baraka iliyojificha,” alisema.

Aidha, aligusia mzozo mkubwa wa kifamilia aliokumbana nao kati ya mwaka 2022 na 2023, ambao ulimpelekea kuweka mipaka imara iliyomsaidia kupata utulivu wa maisha.

"Nilijikuta kila mara nikirudi kwa watu waliokuwa wakinishusha thamani. Tukikutana kwenye hafla tunaendelea kana kwamba hakuna kilichotokea. Haichukui hata wiki kabla ya ugomvi mwingine. Nikajua, aaah, kuna shida hapa," Akothee aliandika.

Sasa, anasema maisha yake yamejaa amani na mwangaza mpya. Aliwahi kumuuliza Nelly Oaks kwa nini siku hizi haishii tena hospitalini hata anapochoka kazini, naye akamjibu: “Kwa sababu sasa uko na amani na hakuna anayekuchochea.”

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved