logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mlinzi wa waziri Matiang'i amuua mkewe kabla ya kujitoa uhai

Mlinzi wa waziri Matiang'i amuua mkewe kabla ya kujitoa uhai

image
na Radio Jambo

Habari07 April 2021 - 05:51

Muhtasari


• Mashahidi walisema afisa huyo alifika nyumbani karibu saa tatu jioni na kumkuta mkewe akila chakula cha jioni na mabishano kuhusu uamuzi wake wa kuhama yakaibuka.

•Aliondoka kabla ya kurudi nyuma na kumpiga risasi mama huyo kifuani mara nane.

Hudson Wakise, alimpiga risasi na kumuua mkewe, Pauline Wakasa, kabla ya kujigeuzia bunduki. Picha: HISANI

Afisa wa polisi anayehudumu katika ofisi ya waziri Fred Matiang’i ameripotiwa kujitoa uhai baada ya kumuua mkewe ambaye alikuwa polisi wa trafiki.

Inspekta mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba afisa huyo wa GSU, Hudson Wakise, alimpiga risasi na kumuua mkewe, Pauline Wakasa, kabla ya kujigeuzia bunduki na kujifyatulia risasi.

Maafisa waliozuru eneo la tukio walipata miili hiyo sebuleni.

Mutyambai ambaye aliomboleza vifo hivyo alisema kwamba huenda wawili hao walizozana ya ufyatulianaji wa risasi.

Wakise, ambaye hakuwa kazini tangu Aprili 1, alirudi kazini Aprili 6 lakini aliondoka saa tisa alasiri na kurudi nyumbani nje ya kambi ya GSU huko Ruaraka ambapo tukio hilo lilitokea.

Walikuwa wamezozana kuhusu hatua ya Pauline kuhama kambi ya GSU.

Anasemekana kuhamia kwa nyumba mpya siku ya Jumamosi.

Watoto wao wawili wa miaka mitano na miwili walinusurika kisa hicho cha kuhuzunisha.

Mashahidi walisema Wakise alifika nyumbani karibu saa tatu jioni na kumkuta mkewe akila chakula cha jioni na mabishano kuhusu uamuzi wake wa kuhama yakaibuka.

Kisha akaondoka kabla ya kurudi nyuma na kumpiga risasi mama huyo kifuani mara nane.

Alijigeuzia bunduki kwenye kidevu na kujipiga risasi iliyopasua kichwa chake.

Pauline alikuwa afisa wa trafiki katika eneo la Kilimani. Alikuwa bado katika sare zake rasmi wakati wa tukio hilo.

Miili hiyo baadaye ilihamishiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Waziri Matiang'i siku ya Jumatano aliomboleza maafisa hao wawili akitaja vifo vyao kama tukio la kusikitisha.

"Nimeumizwa sana na tukio baya la afisa Hudson Wakise na mkewe Pauline Wakasa wote wawili maafisa wa polisi wachanga na mahiri waliokuwa na maono mazuru mbeleni yaliozikwa kutokana na kisa cha kusikitisha," Matiang’i alisema kwenye tweet yake.

"Ni ishara kuhusu changamoto za kisaikolojia miongoni mwa baadhi ya maafisa wetu wachanga na hatuna budi ila kuangazia hali hii zaidi. Risala zangu za dhati kwa familia zao na marafiki."

Polisi waliamua kuwa kisa hicho ni mauaji na kujitia kitanzi na kutangaza kuwa kesi hiyo imefungwa kwa sasa.

Matukio kama haya ya mauaji na kujitoa uhai yanaongezeka katika idara ya polisi.

Wataalam wanasema matukio haya yanasababishwa na changamoto za kikazi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved