logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Maandamano mitandaoni baada ya Joho na Junet kupakia video ya Ruto iliyofanyiwa ukarabati

Video hiyo iliyofanyiwa ukarabati kumuonyesha Ruto akizungumza maneno ya chuki dhidi ya jamii fulani za Kenya.

image
na Radio Jambo

Habari03 August 2022 - 04:39

Muhtasari


•Joho, Junet na Etale walikabiliwa na ghadhabu za wanamitandao waliowashutumu kwa kueneza propaganda dhidi ya naibu rais William Ruto.

•Watatu hao walipakia video iliyofanyiwa ukarabati kumuonyesha Ruto akizungumza maneno ya chuki dhidi ya makabila mbalimbali ya hapa nchini.

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, mbunge wa Suna East Junet Mohamed na Mkurugenzi wa mawasiliano katika ODM Philip Etale walikuwa mada kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu Jumanne baada ya kuchapisha video zilizofanyiwa ukarabati.

Wanachama hao wa ODM walikabiliwa na ghadhabu za wanamitandao waliowashutumu kwa kueneza propaganda dhidi ya naibu rais William Ruto.

Jumanne alasiri, watatu hao walipakia video iliyofanyiwa ukarabati kumuonyesha Ruto akizungumza maneno ya chuki dhidi ya makabila mbalimbali ya hapa nchini.

"Madharau na Vitisho kwa watu wa Central , Western na Nyanza yataisha Tarehe Tisa mwezi huu !! Ni aibu iliyoje kwa Naibu rais wa nchi ya jamii nyingi kuzungumza hivi!" Junet aliandika chini ya video aliyopakia kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Video hiyo iliyodondolewa kutoka kwa hotuba ya naibu rais katika kaunti ya Uasin Gishu pia ilichapishwa kwenye akaunti rasmi ya Twitter ya chama cha ODM.

Katika video hiyo, Ruto alikuwa akiwahutubia wakazi wa Uasin Gishu kwa lugha ya Kalenjin kabla ya kubadilisha na kuwahutubia kwa Kiswahili.

Radio Jambo imeweza kubaini kuwa baadhi ya maneno kutoka kwa hotuba ya mgombea urais wa Kenya Kwanza yalikuwa yametolewa katika video iliyopakiwa na wanasiasa hao.

Baadhi ya maneno ambayo naibu rais alisema kwa lugha yake ya Kalenjin pia yalikuwa yametafsiriwa vibaya.

Ili kuondoa shaka, msemaji wa timu ya kampeni ya Ruto, Hussein Mohamed alichapisha video ya hotuba halisi ya naibu rais kabla ya kufanyiwa ukarabati.

"Video asili kutoka kwa mkutano wa Eldoret. Leo, watu/Hustler Nation, wamepangwa kwa makundi ya  masilahi ya kiuchumi, SI makabila!" Hussein aliandika chini ya video halisi ambayo alipakia Twitter.

Tazama video halisi hapa:- 

Wanamitandao wenye ghadhabu waliwakosoa Junet, Joho na Etale na kuwataka kujiepusha na matendo yanayoweza kuwapiganisha Wakenya.

Baadhi ya wanamitandao walichukua hatua ya kuripoti akaunti za watatu hao pamoja na ile ya ODM wakitaka zifutwe Twitter.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved