
KINARA wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amemuonya rais William Ruto dhidi ya kuwapuuza vijana wa kizazi cha Gen Z.
Akizungumza Ijumaa Februari 21, Kalonzo
alisema kwamba mustakabli wa taifa la Kenya uko mikononi mwa Gen Z akisema
kwamba vijana hao ndio wataamua jinsi uchaguzi mkuu wa 2027 utakavyokuwa.
Alimtaka rais Ruto kutowapuuzilia mbali Gen
Z kama watu wa kufoka kwenye mitandao ya kijamii, akisema kwamba sauti za ni za
maana katika kuathiri matokeo na matukio mbalimbali nchini.
Kinara huyo mwenza wa Azimio alitolea mfano
jinsi matokeo ya AUC yalivyofanyika kupelekea Raila Odinga kushindwa, akisema
kwamba ni kutokana na pingamizi kali ambazo zilikumba ugombeaji wa Odinga
kutoka kwa Gen Z mtandaoni.
Alimlaumu Ruto kwa kutotilia maanani sauti
na maoni ya Gen Z kupelekea vijana hao kuanzisha kampeni dhidi ya Odinga kwenye
kinyang’anyiro cha AUC ambapo walishinda baada ya Odinga kufeli.
“Ninaweka lawama kwa Rais William
Ruto, ambaye ndiye aliyekuwa mpiga kampeni mkuu. Alikuwa na nia tofauti kwamba
labda akimskuma Raila atakuwa na wakati rahisi zaidi, lakini hakujua itakuwa
vigumu sana. Na pia ikumbukwe vijana wa Gen Z wako na uwezo wa kuloby, and they
lobbied directly. Hii ndiyo sababu nyingine kuu ya Raila kushindwa,” Kalonzo alisisitiza.
Alisisitiza kuwa bendera ya Kenya
iliyobebwa na Raila katika kampeni yake inaashiria utawala ule ule ambao
ulishutumiwa kuwaua waandamanaji wasio na silaha, haswa waandamanaji wa Gen Z
ambao walikabiliwa na nguvu za kikatili na vyombo vya usalama.
Ghasia zinazoshukiwa kufadhiliwa na
serikali dhidi ya wanaharakati vijana, alisema, zilipunguza kwa kiasi kikubwa
uungwaji mkono wa kuwania kwa Raila, kwani nchi nyingi zilihusisha mbio zake na
utawala unaotawala.
“Wewe, Raila hakuwa Raila; alikuwa
mgombea wa Jamhuri ya Kenya. Sasa watu wanaangalia ile bendera ya Kenya Raila
alikuwa nayo pale ni the same bendera watoto walikuwa wanabeba na chupa ya maji
na kufanya valid demonstrations na kuuawa, with no valid explanation. Kwa hivyo
wakasema ni yule rais aliua watoto ndiye amewakilisha mgombeaji hapa,” Kalonzo alisema.