

HUENDA mji wa Thika ambao ni makao makuu ya kaunti ya Kiambu ukawa jiji la 6 nchini Kenya baada ya Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret baada ya ripoti kuwasilishwa na gavana katika bunge la kaunti.
Azma hiyo inayolenga kupandishwa hadhi kwa
Thika kutoka mji hadi jiji imeshika kasi na sasa wawakilishi wadi watatakiwa
kujadili ripoti hiyo kabla ya kuuwasilisha mswada kwenye bunge la seneti
kujadiliwa.
Ikikabidhiwa, litakuwa jiji la sita nchini
na la kwanza katika eneo la Kati mwa Kenya.
Ripoti na hati hiyo ilitayarishwa na kamati
ya muda iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Seneta Sylvia Kasanga, ikiangazia
utayari wa mji huo kuwa jiji.
Ilikabidhiwa kwa Spika wa Bunge la Kaunti
na Karani wakati wa hafla iliyoandaliwa katika Jumba la Wahitimu wa Chuo Kikuu
cha Mount Kenya mjini Thika jana.
Wamatangi alionyesha matumaini kuwa mji
utapata kupandishwa hadhi, akiongeza kuwa mabadiliko hayo yatafungua fursa mpya
za maendeleo na ukuaji wa uchumi.
Alisema mji huo una uwezo wa kuvutia
uwekezaji mkubwa na kuzalisha ajira kutokana na eneo lake la kimkakati, na
kuongeza kuwa hadhi ya jiji itaufanya mji huo kuvutia zaidi ya Sh6 bilioni kila
mwaka kwa ajili ya kuendeleza miundombinu na kutoa ajira zaidi ya 50,000
kupitia viwanda na teknolojia.
"Tunatumai kuwa haitachukua muda
mrefu kabla ya kupata jiji katika Kaunti ya Kiambu, la kwanza katika eneo la
Kati. Tumeingia kwenye mchakato wa kutunga sheria, ambao utaongezeka. Thika
ikishakuwa jiji, itakuwa na uwezo wa kuvutia uwekezaji, maendeleo na kubuni
nafasi za kazi. Pia itapunguza shinikizo katika jiji la Nairobi,” alisema gavana Wamatangi.
Kasanga alisema ripoti hiyo ni ya kina,
akisema ilianza kwa ushirikishwaji wa wananchi miongoni mwa wananchi kabla ya
kuandika ripoti.
Viongozi wa eneo hilo, wakiongozwa na Naibu
Spika John Njiru, ambaye pia ni MCA wa Wadi ya Hospitali, walisema hadhi ya
Jiji itasababisha nafasi kubwa za kazi kwa wenyeji.
Alitoa wito kwa wakazi kuunga mkono
mchakato huo, akisema wanaweza kufaidika pakubwa.

