
CHAMA cha ODM kimetoa tamko rasmi kuhusu kuhangaishwa na tafrani inayoendelea katika maigizo ya kitaifa kaunti ya Nakuru ambapo shule ya upili ya wasichana ya Butere imezua gumzo la kitaifa kufuatia igizo lao la ‘Echoes of War’.
Kupitia ukurasa wao wa X, ODM imesuta vikali serikali kwa kuingilia ubunifu wa wanafunzi katika drama za maigizo ya shuleni.
ODM ilisema kwamba serikali haifai kuingilia
kati katika ubunifu wa maigizo ya wanafunzi, ikitolea mfano jinsi wanafunzi
waliigiza kuhusu uongozi dhalimu wa Afrika Kusini katika filamu maarufu ya Sarafina.
“Wengi wetu ambao tulikua katika enzi ya
ukombozi wa pili nchini Kenya tunaelewa kabisa igizo maarufu la Afrika Kusini
la Sarafina. Ilijikita katika wanafunzi wa shule wakisimama kidete kupinga
apartheid na udhalimu kwa jumla,” ODM
ilisema.
“Funzo kubwa kutoka kwayo ni kwamba hata
sauti za Watoto wa shule zina umuhimu, na kwa kweli kutokana na kutokuwa na
hatia na usafi kwao, sauti zao ni za umuhimu mkubwa katika kuendesha mjadala wa
kitaifa,” waliongeza.
Kwa kuonekana kupinga waziwazi igizo la shule
ya wasichana ya Butere la Echoes of War, kupitia mahakama na hata kutuma polisi
kutupa vitoza machozi katika shule walimokuwa huko Nakuru, ODM ilisema kuwa
serikali ni sawa sawa imejipiga risasi mguuni.
“Taifa limefuatilia kwa mshangao tafrani
inayojiri katika kongamano la kitaifa la maigizo jijini Nakuru ambapo serikali
waziwazi imeingiza baridi kutokana na igizo la Butere Girls lenye mada ‘Echoes
of War’”
“Katika Ushahidi wote ambao tuko nao
kuhusu kukosekana kwa umakinifu kwa uongozi huu, serikali imejipiga risasi
mguuni kwa kujaribu kuzima sauti za wasichana wadogo wenye sare za shule,”
ODM iliongeza.
ODM ilisema kwamba kunaibuka maswali magumu
wakati serikali inaonekana kuingiwa woga na Watoto wadogo wa shule ambao
wanajaribu kuonyesha talanta yao katika uigizaji.
“Tungependa kulaani vikali kunyanyaswa
kwa wanafunzi wa Butere Girls, wanahabari na hata watu wengine waliokwenda
kuhudhuria na tunajiunga na Wakenya wengine kuitaka serikali kuwapa wanafunzi
fursa ya maonyesho yao kama wengine,” ODM
ilimaliza.
Taarifa ya ODM inajiri saa kadhaa baada ya mwandishi wa igizo hilo, Cleophas Malala kudaiwa kukamatwa huku polisi wakitupa vitoza machozi katika shule moja walimoweka makaazi wanafunzi wa Butere.