logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kalonzo: Sina Nia ya Kujiunga na Serikali ya Ruto

Kalonzo alikanusha madai kwamba ana mpango wa kufuata nyayo za kiongozi wa ODM Raila Odinga na kujiunga na serikali ya Rais Ruto.

image
na Tony Mballa

Habari30 June 2025 - 09:10

Muhtasari


  • Kalonzo alikiri kuwa Wakenya wanafanya kazi kwa bidii, lakini akakemea uporaji na uharibifu wa mali, huku akihoji ni nani waliohusika kupanga vurugu hizo.
  • Alizungumzia hali ya taharuki inayoongezeka nchini, akitaja tukio la kuuawa kwa Albert Ojwang’ kama ishara ya kilio kikuu miongoni mwa vijana.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amemtaka Rais Ruto ajiuzulu mamlakani, akikanusha vikali uvumi wa kuwa ana mpango wa kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza.

Kalonzo alikanusha madai kwamba ana mpango wa kufuata nyayo za kiongozi wa ODM Raila Odinga na kujiunga na serikali ya Rais Ruto.

Alitoa matamshi hayo siku ya Jumatatu wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini.

“Ushauri wangu kwake (Rais William Ruto) ni kwamba ajiondoe mamlakani pamoja na serikali yake yote,” Kalonzo alisema.

Viongozi wa upinzani Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka

“Watu wengi wanafikiri ati Kalonzo anaweza kushawishiwa na Raila aende kwa Ruto — wasahau kabisa! Mimi nitakuwa mahali wananchi wako, na nimetambua hii ndiyo njia bora ya kufanya mambo,” aliongeza.

Aliwalaumu baadhi ya watu ndani ya serikali kwa uporaji wa rasilimali za umma.

“Wamesema hawataki kudharauliwa kama vijana. Wengine wanavaa saa za shilingi milioni mbili, na wanajua hilo ni kutokana na uporaji wa mali ya Wakenya,” alisema.

Kalonzo alikemea jinsi serikali ilivyoshughulikia maandamano ya hivi majuzi, akidai walipeleka wahuni kuanzisha vurugu.

“Waliharibu maandamano ya amani kwa kuleta wahuni. Waandamanaji wa Gen Z hawakuwa na uhusiano wowote na uhalifu uliopangwa,” alisema.

Alisisitiza kuwa vurugu hizo zilielekezwa kwa makusudi kwenye maduka yanayomilikiwa na jamii ya Wakikuyu, akidokeza kuwa ilikuwa mikakati ya serikali ya Kenya Kwanza.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka akihudhuria hafla ya chama hicho 

“Kenya Kwanza, ikiongozwa na William Ruto, iliandaa kile tulichokiona. Hao ‘wahuni’ walilenga mahsusi maduka yanayomilikiwa na jamii moja. Kulikuwa na mpangilio na ufuatiliaji,” aliongeza.

Kalonzo alikiri kuwa Wakenya wanafanya kazi kwa bidii, lakini akakemea uporaji na uharibifu wa mali, huku akihoji ni nani waliohusika kupanga vurugu hizo.

Alizungumzia hali ya taharuki inayoongezeka nchini, akitaja tukio la kuuawa kwa Albert Ojwang’ kama ishara ya kilio kikuu miongoni mwa vijana.

“Nchi iko katika hali ya matatizo — hali ambayo, kusema kweli, ni ya hatari. Tangu mauaji ya Albert Ojwang’ ndani ya kituo cha polisi, Wakenya wamejitokeza kwa wingi. Mimi mwenyewe nilienda kuadhimisha siku hiyo muhimu ya vijana,” alisema.

Alisema vijana, hasa wa kizazi cha Gen Z, wanaandamana kupinga kudharauliwa na wanatambua hali ya ukosefu wa usawa unaochochewa na hatua za serikali.

“Wakenya wanafanya kazi kwa bidii sana. Lazima tukemee uporaji na uharibifu wa mali. Lakini pia tujiulize: ni nani waliopanga mambo haya? Sisi, kama wapinzani, hatuna namna — wao wanatumia rasilimali za serikali. Nia ya vijana wa Gen Z ni safi,” alisema.

Kalonzo alibainisha kuwa maandamano hayo hapo awali yalikuwa na lengo la kuwa ya amani na akatoa wito wa kusitishwa kwa ukatili dhidi ya waandamanaji.

Kalonzo Musyoka

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved